Tuesday, March 14, 2017

SERIKALI MKOANI RUVUMA YATENGA MILIONI 335.6 KWA VIKUNDI VYA VIJANA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

KATIKA kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuviwezesha vikundi vya vijana na wanawake hapa nchini, mkoa wa Ruvuma kupitia halmashauri zake nane zilizopo mkoani humo imetenga shilingi milioni 335.6 kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 ili vikundi hivyo viweze kujiinua kiuchumi na kusonga mbele kimaendeleo.

Katika fedha hizo tayari mikopo ya shilingi milioni 90.5 imetolewa kwa vikundi vya vijana 2,619 vyenye wanachama 1,292 ambao wamenufaika na mikopo ya fedha za mfuko wa maendeleo ya vijana pamoja na fedha za mapato ya ndani ya halmashauri husika ndani ya mkoa huo.

Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na vijana 672,540 sawa na asilimia 48 ya wakazi wa mkoa huo wapatao milioni 1,376,891 kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na wastani wa ongezeko la watu kila mwaka.

Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu tawala wa mkoa huo, Bwai Biseko alipokuwa akitoa taarifa ya shughuli za maendeleo ya vijana mkoani hapa kwenye mafunzo elekezi ambayo yalijumuisha vijana hao kutoka mikoa mitatu ya Ruvuma, Lindi na Mtwara yaliyofanyika katika Manispaa ya Songea mjini hapa.


Biseko alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo cha kahawa, korosho, mahindi, mpunga upandaji miti ya mbao, kilimo cha soya, mbaazi, uvuvi, bustani za mboga mboga pamoja na biashara za kuuza bidhaa ndogo ndogo kwa lengo la kukuza maisha yao yaweze kusonga mbele kupitia mikopo hiyo wanayoipata kwenye vikundi vyao.

Aidha alieleza kuwa mkoa huo unaendelea kutekeleza majukumu yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vijana hao, kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ambavyo kupitia halmashauri za wilaya vimetambuliwa na baadhi yake huendelea kupewa mikopo.

Akizungumzia juu ya utengaji wa maeneo ya shughuli za vijana, mikopo ya mfuko wa maendeleo ya vijana pamoja na asilimia tano ya mapato ya ndani ya halmashauri, Biseko aliongeza kuwa halmashauri zote za mkoa huo wilaya ya Madaba, Mbinga vijijini, Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Songea vijijini, Manispaa ya Songea na halmashauri ya mji wa Mbinga tayari zimetenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana na akina mama.

Kadhalika alibainisha kuwa halmashauri ya Madaba imetenga shilingi milioni 12.5 kwa vikundi saba kati ya vikundi 21, Manispaa ya Songea imetenga shilingi milioni 26.4 na vikundi 10 vimepata mkopo wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya biashara ndogo ndogo, mama lishe na boda boda na tayari imetenga ekari tisa na kutolewa kwa wafanyabiashara wadogo katika kata ya Msamala, Majengo na Ruhuwiko.

Alitaja halmashauri nyingine kuwa ni Songea vijijini iliyotenga na kutoa shilingi milioni 10 kwa vikundi vitano kati ya 255 vya vijana vilivyopo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo.

Vilevile halmashauri ya wilaya ya Nyasa katika bajeti yake imetenga shilingi milioni 25.7 ambazo bado hazijapelekwa kwa wahusika na kwamba tayari imetenga pia eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo cha zao la Cocoa, umwagiliaji mpunga na kilimo cha zao la kahawa.

Biseko alisema kuwa halmashauri ya mji wa Mbinga imetenga shilingi milioni 4 na tayari imekwisha toa kwa kikundi cha vijana kimoja kilichopo mjini hapa, Namtumbo imetenga shilingi milioni 57 na fedha iliyotolewa katika fedha hizo tayari shilingi milioni 12 zimekwenda kwa vikundi 21 sambamba na kutenga eneo la ekari 331.39 katika kata ya Rwinga na Namtumbo kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru alisema kuwa wametenga shilingi milioni 200 ambapo hadi sasa imekwisha toa shilingi milioni 42.097 kwa vikundi 30 na kwamba kati ya vikundi 263 vinavyojishughulisha na usindikaji wa mazao ya chakula, kilimo, useremala, ushonaji na urinaji asali.


Hata hivyo alieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni upungufu wa maofisa vijana kwani mkoa una upungufu wa maofisa sita kati ya wanane wanaohitajika kwenye halmashauri, elimu ya ujasiriamali bado haijawafikia vijana wengi, ukosefu wa soko la uhakika hasa kwa mazao ya chakula na biashara na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha  na kuendesha miradi ya vijana.

No comments: