Wednesday, March 15, 2017

MKANDARASI UJENZI WA BARABARA YA NAMTUMBO HADI TUNDURU ALIFUKUZWA NA SERIKALI KUTOKANA NA KUSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU ALIYOPEWA

Na Muhidin Amri,      
Songea.

WAKALA wa Barabara (TANROAD) mkoani Ruvuma amesema kwamba kuanzia mwezi Januari mwaka 2013 hadi kufikia Januari mwaka huu, ametumia jumla ya shilingi bilioni 2,011,195,000 ikiwa ni gharama ya ulinzi wa mitambo iliyoachwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Progressive Higleig ya kutoka nchini India.

Imeelezwa kuwa gharama hizo zimetokana na kuwalipa askari Polisi waliokuwa wakilinda mitambo ya kampuni hiyo katika maeneo mbalimbali ya mradi kwa kipindi cha miaka minne, baada ya serikali kumfukuza mkandarasi huyo kutokana na kushindwa kujenga barabara ya kutoka wilaya ya Namtumbo hadi Tunduru mkoani hapa kwa kiwango cha lami.

Meneja wa TANROAD wa mkoa huo, Razack Alinanuswe alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake na kuongeza kuwa serikali imeingiza shilingi bilioni 4,319,452,900 baada ya kuuza mitambo hiyo kwa njia ya mnada kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali.

Alisema kuwa baada ya serikali kumfukuza mkandarasi huyo kutokana na kushindwa kwake kufanya kazi hiyo aliyopewa, ililazimika kushikilia mitambo yake na Wakala huyo wa barabara mkoani hapa na kubeba jukumu la kuilinda kwa muda wote kwa kutumia Jeshi la Polisi ambalo lilifanya kazi kwa uadilifu mkubwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto mbalimbali.


Pia Alinanuswe alifafanua kuwa serikali iliuza mitambo hiyo kwa njia ya mnada kwa lengo la kuepuka ongezeko la gharama kubwa kama vile ulinzi, pamoja na kuendelea kusimamia sheria ya hifadhi ya barabara ili kuhakikisha kwamba watu hawajengi katika hifadhi ya barabara hiyo.  

Meneja huyo alisema kuwa licha ya serikali kukamilisha ujenzi wa barabara za lami kutoka Songea hadi Mbinga yenye kilometa 96 Songea hadi Namtumbo kilometa 68 na Namtumbo kwenda Tunduru hadi Mangaka barabara hizo kuna mizani mpya mbili ambazo zimejengwa kwa ajili ya kudhibiti magari yasiweze kuzidisha uzito ambazo zimejengwa katika kijiji cha Lipokela wilayani Songea na Luhimba kuelekea Tunduru.

Alisema kuwa katika barabara kuu ya Tunduru Mangaka kuna mzani mmoja katika kijiji cha Sisi kwa Sisi ambao umekwishajengwa, lakini mkandarasi bado anamalizia marekebisho machache yaliyobakia ili aweze kukabidhi tayari kwa kuanza kutumika.

Vilevile alibainisha kuwa mkoa wa Ruvuma changamoto kubwa inayokabiliana nayo katika kazi za ujenzi wa miradi ya barabara za lami ni upungufu wa changarawe, udongo mzuri kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara hizo jambo ambalo wataalamu hulazimika kuchanganya kifusi na saruji au chokaa ili kuongeza ubora.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa Wakala wa barabara mkoani Ruvuma, alieleza kuwa tatizo lingine ni upungufu wa fedha kwani mkoa umekuwa ukipokea fedha pungufu kuliko mahitaji husika, hasa kwa ajili ya matengenezo ya madaraja na shughuli zingine za utawala.


Hata hivyo alisema kuwa mbali na matatizo hayo pia kwa muda mrefu mkoa unakabiliwa na uwepo wa uwezo mdogo wa wakandarasi wa kazi za ujenzi wa barabara za lami, pia wakandarasi hao kuchelewa kujipanga kwa vifaa vya mitambo ya ujenzi na kokoto za matengenezo ya barabara hizo.

No comments: