Friday, March 3, 2017

MUHONGO AKUTANA NA KAMPUNI ZA UTAFUTAJI NA UCHIMBAJI MAFUTA NA GESI ASILIA NCHINI

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mbele katikati) akiongoza mkutano na wawakilishi wa Kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini mkoani Mtwara hivi karibuni.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo upande wa kulia akizungumza wakati wa mkutano na Kampuni zinazojihusisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini uliofanyika Madimba, mkoani Mtwara hivi karibuni. Kushoto ni Kaimu Kamishna msaidizi wa nishati sehemu ya Petroli, Mwanamani Kidaya.

Mwakilishi kutoka Kampuni ya Ophir Energy, Halfan Halfan (katikati) akielezea maendeleo ya shughuli zinazofanywa na kampuni yake wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Na Mwandishi wetu,
Mtwara.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kwamba mikutano ya kila baada ya miezi mitatu na kampuni zinazojihusisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia hapa nchini, itakuwa ikifanyika maeneo mbalimbali nchini hususan kwenye rasilimali husika.

Waziri Muhongo aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Mtwara wakati wa mkutano wake na wawakilishi wa kampuni hizo, uliofanyika kwenye Kituo cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani humo.

Alisema kuwa mikutano hiyo mara zote ilikuwa ikifanyika Jijini Dar es Salaam hivyo ili kuweza kuleta tija zaidi ni vyema ikafanyikia kwenye maeneo yenye gesi asilia na baadaye siku za usoni itafanyika kwenye maeneo yatakayogundulika kuwa na mafuta.


Kadhalika aliongeza kuwa kila baada ya miezi mitatu kumekuwepo na utaratibu wa kukutana kwa ajili ya kutathimini maendeleo ya miradi husika na kila kampuni itakuwa ikiwasilisha ratiba yake ya kazi ambayo itajadiliwa.

“Hii mikutano kila kampuni itakuwa ikitupatia ratiba yake ya kazi, tunaijadili na kushauriana endapo kama wana matatizo tunatafuta suluhisho,” alisema Waziri Muhongo.


Waziri Muhongo alisema shughuli za utafutaji, uvunaji na uendelezaji wa gesi asilia na mafuta zinaendelea vizuri huku majadiliano mbalimbali yakiendelea kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo.

No comments: