Saturday, March 25, 2017

MHANDISI IDARA YA UJENZI MBINGA ATUMBULIWA KWA MAKOSA YA UZEMBE NA UBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa idara ya ujenzi wilayani  humo, Anyitike Kasongo kutokana na kubainika kufanya makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umm

Anyitike Kasongo.
Aidha imeelezwa kwamba kusimamishwa huko ambako ni kwa muda usiojulikana kunalenga kupisha uchunguzi na baadaye atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito alisema hayo alipokuwa akizungumza juzi na waandishi wa habari ofisini kwake.

Samandito alisema kuwa sababu ya kusimamishwa huko anadaiwa kufanya ubadhirifu na wizi wa mali za umma katika kazi ya ujenzi wa kibanda cha mlinzi chenye thamani ya shilingi milioni 19,000,000 kwenye nyumba ya kuishi Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga ambayo imejengwa mtaa wa Kipika mjini hapa.


Mkurugenzi huyo alisema kuwa Kaimu Mhandisi Kasongo amesimamishwa kazi kwa sababu pia ya kufanya uzembe na kutotekeleza majukumu yake ya kazi alizopewa ipasavyo, jambo ambalo limesababisha hata mwajiri wake apate hasara kutokana na kibanda hicho kujengwa chini ya kiwango.

Vilevile ananyoshewa kidole kwamba alifanya mapokezi ya vifaa ambavyo hakuvipeleka katika eneo la ujenzi wa kibanda hicho na kwamba jambo hilo lilibainika baada ya kufanya ukaguzi wa ndani.

Pamoja na mambo mengine uchunguzi uliofanywa kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa Mhandisi huyo katika sehemu ya fedha hizo za ujenzi wa kibanda hicho anadaiwa kuzifanyia matumizi tofauti na miongozo aliyopewa shilingi milioni 7,254,500 kwa lengo la kujinufaisha kwa matakwa yake binafsi.

“Fedha hizi zilikuwa ni sehemu ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa kibanda hiki lakini muda mwingi alikuwa akionekana yeye akifika hapa dukani kuja kuchukua vifaa vya ujenzi sasa tunashangaa kwa nini ameshindwa kukamilisha ujenzi huu kwa viwango vinavyotakiwa wakati kuna vifaa vingi alivichukua”, kilisema chanzo chetu.

Mhandisi Kasongo alipotafutwa na mwandishi wetu ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya jambo hilo hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Hata hivyo baada ya kurejeshwa kazini mwezi mmoja uliopita kutokana na kushindwa kusimamia kikamilifu mradi wa ujenzi nyumba za walimu katika kata ya Kitura wilayani hapa, hii ni mara ya pili kwa Mhandisi huyo kuchukuliwa tena hatua ya kusimamishwa kazi na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga kufuatia kufanya makosa ya ubadhirifu wa vifaa vya ujenzi katika kibanda hicho cha mlinzi.

No comments: