Monday, March 20, 2017

RAIS MAGUFULI AWATAKA WATANZANIA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi leo Jijini Dar es Salaam.
Na Daudi Manongi,  Maelezo.

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Watanzania hapa nchini kuulinda mradi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam ambapo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 188 na kukamilika mwaka 2019. 

Rais Magufuli alisema hayo leo wakati alipokuwa akitoa hotuba yake kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hizo katika eneo la Ubungo Jijini hapa. 

“Tutasimamia fedha hizi kikamilifu ili tuweze kujenga barabara hizi za juu vyema, nawataka Watanzania wenzangu kusimamia mradi huu ipasavyo ili ukamilike haraka na hivyo wizara, mkandarasi na msimamizi wa mradi huu uweze kukamilika na kuleta tija kwa wananchi wetu”, alisisitiza Rais Magufuli. 

Alisema kuwa katika ujenzi wa mradi huo shilingi bilioni 1.9 zinatoka serikalini na bilioni 186 zitatolewa na benki ya dunia. 

Rais Magufuli alisisitiza kuwa nchi ya Tanzania imepata mkopo wa fedha hizo kwa sababu inaaminika katika kukopesheka na kurejesha kwa wakati madeni inayokopa huku akiiomba benki hiyo kuendelea kuikopesha hata katika miradi mingine ya maendeleo ya wananchi. 

Vilevile alifafanua kuwa mkopo huo kutoka benki ya dunia una riba ya asilimia 0.5 na utalipwa ndani ya miaka 40 hivyo ni vyema sasa kuendelea kushirikiana na benki hiyo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi hapa nchini. 

Pamoja na hayo amewataka Watanzania kuendelea kulipa kodi itakayowezesha ili serikali iweze kuendelea kutekeleza miradi mingine na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa sura pekee kwa jiji la Dar es Salaam na kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa. 

Kwa upande wake Rais wa benki ya dunia Dkt. Jim Yong Kim ametoa shukrani kwa serikali ya Tanzania na kusema kuwa ameshawishika kuja nchini humo baada ya kusikia vongozi wengi wa dunia wakisifia jitihada za Rais Magufuli katika kuunda upya serikali yake ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi na kuwekeza katika kujenga miundombinu na kukuza sekta ya elimu. 

“Tanzania inaelekea kuwa Taifa la watu wa kipato cha kati miaka nane ijayo na kila mtu kuwa na bima ya afya, elimu bora na muono mzuri wa mbele na njia pekee ya kufika huko ni kujitegemea na kutumia rasilimali za nyumbani katika mkakati bora kabisa na hivyo kupunguza kabisa misaada ya nje ambayo imeshuka hapa nchini kwenu”, alisema Dkt. Jim Yong Kim.

Hata hivyo alisisitiza kuwa benki ya dunia itaendelea kusimama pamoja na Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kufanya kazi pamoja. 

No comments: