Saturday, March 18, 2017

MRADI WA MAJI KIGONSERA WAHARIBIWA NA MAFURIKO YA MVUA


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa mafuriko ya mvua yaliyosababisha kuzolewa kwa mradi wa maji Kigonsera uliopo katika kata ya Kigonsera wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, uharibifu uliotokea umesababisha hasara ya shilingi milioni 15,000,000 ikiwa ni gharama sasa inayotakiwa kufidia ujenzi wa miundombinu ya maji ambayo imeharibika.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yohanes Nyoni alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya tukio hilo ambapo alieleza kuwa lilitokea Machi 6 mwaka huu katika kata hiyo.

Nyoni alifafanua kuwa sababu kubwa iliyosababisha mradi huo kuharibiwa na mafuriko hayo inatokana na uchafuzi wa mazingira katika chanzo hicho cha maji kwani baadhi ya wananchi wameweka makazi ya kudumu karibu na chanzo na kuendesha shughuli za kilimo.

Alisema kuwa hali hiyo husababisha nyakati za masika udongo kumomonyoka hatimaye matope hujaa kwenye chanzo na mawe makubwa yaliyobebwa na mafuriko kuvunja miundombinu husika ya mtego wa maji kutokana na kukosekana kwa uimara wa ardhi.


Pia alieleza kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi hao kukata miti rafiki ya maji na ambayo pia imekuwa ikitunza ardhi inayozunguka chanzo hicho jambo ambalo husababisha chanzo kuzolewa na wananchi kukosa maji.

Alisema kuwa timu ya wataalamu imekwenda katika eneo la tukio na kubaini uharibifu huo ambapo wameshauri kwamba katika kuweza kuwanusuru wananchi wa Kigonsera kukosa maji kwa muda mrefu ni vyema sasa, yakachukuliwa maji kutoka chanzo cha Mkako na kuyagawa katika sehemu mbili ili kuweza kulisha wananchi hao kwa muda wakati upembezi yakinifu ukiendelea kufanyika juu ya kukarabati chanzo hicho kilichoharibiwa na mafuriko hayo.

Vilevile aliongeza kuwa tathimini iliyofanyika ili kuweza kunusuru hali hiyo imebainika kuwa kutoka kwenye mtandao mkuu wa mradi wa maji Mkako mpaka katika mtandao mkuu wa maji Kigonsera baada ya kufanya vipimo vya umbali wa bomba, ujenzi wake pamoja na usimamizi jumla ya shilingi milioni 5,685,000 zinahitajika ili maji yaweze kufika kwenye matenki ya kuhifadhia maji katika mradi wa maji Kigonsera.

Endapo zitapatikana fedha hizo na kazi hiyo kufanyika, wananchi hao watakuwa wameondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.


Kwa ujumla mradi wa maji Kigonsera ambao umeharibiwa na mafuriko ya mvua ulianza kujengwa mwezi Agosti mwaka 2012 na kukamilika ujenzi wake mwezi Machi 2013 chini ya Mpango wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RWSSP) ambapo uligharimu shilingi milioni 479,153,257 ikiwa ni gharama za ujenzi wa mradi wote.

No comments: