Sunday, March 19, 2017

RC RUVUMA AGEUKA MBOGO MHANDISI MSHAURI ANUSURIKA KUMWEKA MAHABUSU

Gari la halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma lenye namba STK 7456 likipita kwa shida katika barabara ambayo alipewa kujenga kwa kiwango cha lami kutoka kijiji cha Longa, Kipololo hadi Litoho wilayani humo Mkandarasi wa Kampuni ya Canopies International Tanzania Limited ya Jijini Dar es Salaam na G'S Contractors Company Limited ya kutoka mkoani Iringa tangu mwaka 2015 ambapo ilitakiwa kukamilika ujenzi wake mwaka jana lakini hadi sasa bado haijakamilika na kusababisha kero kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Salum Mjema ambaye ni Mhandisi mshauri na mkaguzi mkuu wa kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kijiji cha Longa, Kipololo na Litoho wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambayo imefadhiliwa na Jumuiya ya nchi za Ulaya (EU) amenusurika kuwekwa mahabusu na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge kwa madai kwamba ameshindwa kusimamia ipasavyo na kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati uliopangwa.

Mkuu huyo wa mkoa aligeuka na kuwa kama mbogo wakati alipokuwa akikagua barabara hiyo juzi kufuatia taarifa iliyomfikia ofisini kwake kwamba mradi huo umekuwa ukisuasua ujenzi wake, licha ya kazi hiyo kupewa wakandarasi wawili wa Kampuni ya Canopies International Tanzania Limited na G’S Contractors Company Limited kushindwa kujenga kwa tabaka la lami barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 24.954 katika kipindi cha kuanzia Septemba 30 mwaka 2015 hadi Desemba 30 mwaka 2016.

Dkt. Mahenge alionekana kuwa mkali na kusikitishwa na hali hiyo huku akishangazwa na wakandarasi hao kulipwa fedha kwa baadhi ya kazi walizofanya huku hatua ya utekelezaji ikiwa bado haijakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

“Hivi sasa naweza nikawaweka ndani tokea barabara hii ianze kujengwa hadi sasa haijakamilika, naagiza viongozi ngazi ya mkoa na wilaya ya Mbinga kwa kushirikiana na Katibu tawala wa mkoa huu fanyeni uchunguzi wa kina juu ya kazi hii ikiwemo na malipo yaliyofanyika, kwani inaonesha ni uchakachuaji mtupu umefanyika na tukibaini haya maovu mliyoyafanya tutawaweka ndani wote watakaokuwa wamehusika kuhujumu mradi huu na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria”, alisema Dkt. Mahenge.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka pia viongozi wa wilaya ya Mbinga kuwa na mazoea ya kutembelea miradi ya maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali na kuacha tabia ya kukaa maofisini, kwani mfano unaonesha kwamba barabara hiyo viongozi walikuwa hawasimamii kwa ukaribu ndio maana utekelezaji wake umekuwa ni wa hovyo.

Dkt. Mahenge aliongeza kuwa mradi huo umekuwa kama shamba la bibi watu kujipatia fedha na kugawana na kwamba hatua zinapaswa kuchukuliwa mapema kuanzia sasa, ili serikali ya Tanzania na wafadhili hao wa Jumuiya ya nchi za Ulaya wasiweze kupata hasara kwa fedha nyingi zinazotumika katika ujenzi wa barabara hiyo.

Kwa upande wake alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya malipo yaliyofanyika kwa wakandarasi hao Kaimu Mhandisi wa ujenzi halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Said Almas alimweleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Mahenge kwamba Kampuni ya Canopies International Tanzania Limited na G’S Contractors Company Limited fedha zilizotumika kuwalipa ni jumla ya Euro 926,966.62 kati ya fedha zilizotolewa Euro milioni 4,834,224.55 ambapo hadi mradi kukamilika kwake zimebakia Euro milioni 3,907,257.93.

Naye Salum Mjema ambaye ni Mhandisi mshauri na mkaguzi mkuu wa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo alikiri kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kwa siku walizopewa, akidai kwamba tatizo hilo limetokana na hali ya hewa mvua kunyesha na kusababisha kazi kusimama kwa muda.

Mjema alimweleza Mkuu huyo wa mkoa kwamba kazi walizozifanya mpaka sasa na kuweza kulipwa fedha hizo ni kusafisha barabara, kuondoa tabaka la juu la udongo, kukata milima na kuandaa maeneo ya kujenga makalvati.

Hata hivyo baada ya kutoa maelezo hayo Dkt. Mahenge alipingana naye na kueleza kwamba, kwa kisingizio cha mvua huo ni wizi na kuficha maovu waliyoyafanya hivyo serikali itakapokamilisha uchunguzi wake na kubaini hujuma zilizofanyika wakandarasi hao watasitishiwa mikataba yao ya kazi na mitambo yao ya kufanyia kazi itakamatwa na kwamba watalazimika kurejesha fedha zote walizolipwa ili tenda ya ujenzi wa barabara hiyo, iweze kutangazwa upya na kumpata mkandarasi mwingine atakayefanya kazi kwa viwango vinavyokubalika.

No comments: