Monday, March 20, 2017

NAPE AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA TUKIO LA UVAMIZI KITUO CHA HABARI CLOUDS MEDIA

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari (hawapo katika Picha) alipofanya ziara katika Chombo cha Habari cha Clouds Media Group leo Jijini Dar es Salaam.
                Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye                       Katikati, akimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya                   Habari  Nchini (MOAT) Reginald Mengi (kulia) alipofanya ziara katika chombo cha Habari leo Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas.
              Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye                       (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Joseph                 Kusaga (wa pili kushoto) alipowasili katika ofisi hizo leo Jijini Dar es Salaam,             wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas (Pembeni             ya Waziri) na wa kwanza kushoto ni Afisa Mahusiano wa Clouds Simon                                                                       Simalenga.
                  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye                  (katikati) akielezwa jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo                vya    Habari Nchini (MOAT) Reginald Mengi (kulia) alipotembelea Ofisi hizo            leo Jijini          Dar es Salaam, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media                                                            Joseph Kusaga.
  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye                   (kushoto) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya                                            Jamii Peter Serukamba (MB).
             Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya jamii wakimsikiliza Mwenyekiti wa              Kamati hiyo (hayupo katika picha) Peter Serukamba (MB) walipotembelea Kituo cha                               Habari cha Clouds leo Jijini Dar es Salaam. 
Na Mwandishi wetu,

WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye ameunda Kamati ya watu watano itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas kuchunguza tukio la uvamizi lililofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika chombo cha habari cha Clouds Media.

Akiongea katika ziara aliyoifanya  leo  Jijini Dar es Salaam  katika chombo hicho Nape alisema kuwa Kamati hiyo itafanya kazi ndani ya masaa 24 kuanzia sasa huku akiwataja wajumbe wengine  kuwa ni Frank Balile, Johanes Neng’ida, Jessy Kwayu na Mabel Mabisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Serikalini (TCRA).

“Kamati hii ipo kwa ajili ya kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ili tuwe na taarifa iliyokamilika na kujua hatua itakayofuata”, alisema Nape.


Aidha Waziri Nape alieleza kuwa kitendo cha uvamizi kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa huyo kipo kinyume na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa kuwa sheria hiyo ipo kwa ajili ya kulinda wanatasnia hao.

Aliongeza na kufafanua kuwa Serikali imesikitishwa na kitendo hicho na ndio maaana akaunda kamati ya uchunguzi itakayokuja na taarifa kamili huku akiwataka wanatasnia ya habari na wananchi kuwa watulivu na kusubiri majibu ya uchunguzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Habari ya Clouds, Joseph Kusaga amemshukuru Waziri Nape kwa kuonyesha ushirikiano na kuwa pamoja katika jambo hilo huku akifurahishwa na namna Serikali inavyowajali wadau wa Habari.  

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) Reginald Mengi amempongeza Waziri huyo kwa hatua ya kuunda kamati ya uchunguzi kwakuaanaamini itatoa matokeo chanya yatakayolinda heshima ya Tasnia ya Habari nchini.

“Uamuzi wa kuunda kamati hii ni jambo la hekima na busara linaloendana na misingi ya taaluma ya habari nasi tutakuwa radhi kuunga mkono hatua  zitachukuliwa katika kulinda uhuru wa habari nchini”, alisema Mengi.

Tukio la kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Mkonda   limetokea usiku wa  Machi 17 mwaka huu.

No comments: