Saturday, March 18, 2017

BUNDI ATUA KWA OFISA USHIRIKA MBINGA MKUU WA WILAYA ASEMA ANACHUNGUZWA ATACHUKULIWA HATUA KALI ZA KINIDHAMU

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba serikali wilayani humo inaendelea kufanya uchunguzi juu ya malalamiko anayolalamikiwa Kaimu Ofisa ushirika wa wilaya hiyo, Kanisius Komba ambayo yanatoka kwa wakulima wa vyama vya ushirika wilayani hapa na pale itakapobainika kuna ukweli juu ya tuhuma anazonyoshewa kidole na wakulima hao hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Cosmas Nshenye.

Aidha Nshenye alifafanua kuwa wakulima wengi wamekuwa wakimtuhumu kwamba amekuwa hatimizi majukumu yake ya kazi za ukaguzi wa vyama hivyo ipasavyo, badala yake anadaiwa kushirikiana na viongozi wa vyama vya ushirika kuhujumu vyama hivyo visiweze kusonga mbele kimaendeleo.

Kadhalika alidai kuwa wanaushirika hao wamekuwa wakimtuhumu kwamba ni mtu ambaye anapenda kushiriki katika vitendo vya rushwa na kupotosha ukweli wa ripoti za ukaguzi wa vyama hivyo.

Hayo yalisemwa na Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alipokuwa akizungumza juzi na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo aliongeza kuwa amekuwa akitoa taarifa hizo za ukaguzi ambazo wakati mwingine hazina viambatanisho vyenye kuonesha uhalisia wa ukaguzi uliofanyika.

“Hamna pasipo na ushirika Mbinga hii asipolalamikiwa, suala hili lipo tunaendelea kulichunguza taarifa za ukaguzi amekuwa akizifanyia ujanja ujanja na amekuwa sio mtu mkweli katika masuala ya ukaguzi analalamikiwa na watu wengi”, alisema Nshenye.

Pia Nshenye alieleza kuwa chama cha ushirika kimojawapo wanachomlalamikia wilayani humo ni Longa AMCOS ambapo wanachama wa ushirika huo katika msimu wa kilimo mwaka 2015 walichukua mkopo wa shilingi milioni 50 kutoka benki ya NMB lakini Wajumbe wa bodi ya ushirika huo kwa kushirikiana na Kaimu Ofisa ushirika huyo, Komba wanadaiwa kushirikiana kwa pamoja kuhujumu fedha hizo.

Alisema kuwa fedha hizo zilikuwa zitumike kununua pembejeo za kilimo kwa ajili ya wakulima katika msimu huo, lakini pembejeo zilizonunuliwa zilikuwa ni za shilingi milioni 14,000,000 tu na fedha zilizobakia hazieleweki zimepelekwa wapi na kufanya kazi gani.

Vilevile alisema kuwa ofisi yake ilipoona malalamiko hayo yamekuwa mengi kutoka katika vyama hivyo vya ushirika vilivyopo wilayani Mbinga, sasa wanafanya uchunguzi ili kuweza kupata ukweli wa malalamiko hayo na wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments: