Sunday, March 5, 2017

WAFANYABIASHARA SONGEA WANYOSHEANA KIDOLE

Na Mwandishi wetu,        
Songea.

KWA nyakati tofauti Wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamelaani kitendo cha baadhi ya Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea kukosa uzalendo na kushindwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, katika kufanikisha suala la ukusanyaji wa mapato yake.

Aidha walisema kuwa badala yake wafanyabiashara hao wamekuwa wakihusika moja kwa moja kushinikiza watu wengine kukataa ongezeko la kodi mpya ya vibanda katika Soko hilo, kwa ajili ya maslahi yao binafsi huku wapangaji wengine wakijinufaisha kutokana na pango wanalopokea jambo ambalo linaisababishia serikali hasara kubwa.

Walisema kuwa kitendo cha wapangaji hao kugomea ongezeko hilo jipya la pango katika vibanda  hivyo linaonesha ni jinsi gani baadhi ya watu wanavyotaka kujinufaisha kupitia migongo ya watu wengine, kwani haiwezekani  Manispaa ya Songea ikapata fedha kidogo  na watu walioingia mikataba kwa kuwatumia madalali wakiendelea kunufaika kuwapangisha watu wengine kwa fedha nyingi.

Hivi karibuni wafanyabiashara wa Soko kuu la Manispaa hiyo walijikuta katika mgogoro mkubwa na uongozi husika wa Manispaa baada ya kugomea bei mpya ya pango inayotakiwa kulipwa kwa Manispaa badala ya madalali ambao wamekuwa wakijinufaisha kupitia mgongo wa nyuma.


Wakizunguza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti mjini hapa walisema kuwa kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao kuchelewa kujaza maombi kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao za kila siku katika soko hilo hakikuwa cha kiungwana kwa sababu wananchi wanakosa  huduma na  mahitaji muhimu ya kila siku.

Walisema kuwa haiwezekani Manispaa ambayo ndiyo mmiliki halali wa vibanda hivyo hupata pango la shilingi 108,000 kwa mwezi wakati wapangaji hupangisha watu wengine kwa fedha nyingi kati ya shilingi 350,000 hadi 450,000 tena bila kuilipia kodi serikalini.

Kassiana Ngonyani (42) mkazi wa Mateka alisema kuwa hatua ya Manispaa kufunga vibanda vya wafanyabiashara katika soko hilo ilikuwa ni jambo jema kwani kwa muda mrefu ilijikuta ikipata hasara kubwa huku baadhi ya watu wakinufaika licha ya kutoingia gharama yoyote.

Ngonyani alieleza kuwa kitendo baadhi ya wapangaji waliokuwa na mikataba na Manispaa kuwapangisha watu wengine hakikuwa sahihi kwani utaratibu unaeleza kwamba mtu mwenye mamlaka halali ya kupangisha ni Manispaa na sio mtu binafsi.

Christian Kanjolonga  yeye mbali na kuupongeza uongozi wa Manispaa hiyo kwa uamuzi wake wa kufunga vibanda hadi pale wafanyabiashara watakapojaza mikataba mipya  alisema kuwa ni uamuzi sahihi na amewataka wananchi wengine kutambua kuwa, serikali ya awamu ya tano  imekuja na mikakati yake hasa katika ukusanyaji thabiti wa kodi au mapato yake.

Aliongeza kuwa tabia ya kufumbiana  macho na kuoneana aibu na wakati mwingine kubebana ndiyo kunakosababisha  Manispaa ya Songea kuwa kati ya halmashauri maskini hapa nchini, licha ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato ambavyo kama vingesimamiwa vizuri vingeweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za kijamii.

“Lazima wananchi wenzangu wanapaswa kuelewa kwamba, serikali ya awamu ya tano ni tofauti kabisa na serikali zilizotangulia ni vyema sasa kujifunza kulipa kodi na maduhuli mengine ya serikali kwa wakati”, alisema Kanjolonga.


Pamoja na mambo mengine hivi sasa wafanyabiashara na wapangaji wa vibanda hivyo vya Soko kuu la Songea, wanaendelea na shughuli zao baada ya kuingia mikataba mipya ya upangaji na Manispaa ya Songea kutokana na kumaliza tofauti zao zilizokuwepo hapo nyuma.

No comments: