Friday, March 3, 2017

SERIKALI YAZUIA UCHIMBAJI MADINI KWENYE MTO MUHUWESI TUNDURU

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza Ofisa Madini Mkazi wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Fredrick Mwanjisi akielezea kuhusiana na shughuli za uchimbaji wa madini ya vito zilizokuwa zikifanyika kwenye mto Muhuwesi wilayani humo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya vito wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wakati alipotembelea eneo la mto Muhuwesi wilayani humo.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

SERIKALI hapa nchini imezuia shughuli za uchimbaji wa madini ya vito katika mto Muhuwesi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hadi hapo taarifa za kitaalamu zitakapotolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la tathimini na ukaguzi husika.

Agizo hilo la kuzuia kazi hiyo kufanyika katika mto huo limetolewa hivi karibuni wilayani humo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara yake kwenye mto huo ili kujionea hali ya eneo hilo kufuatia ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kanje Ally na majeruhi mmoja ambao waliingia na kuanza kuchimba ndani ya mto huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa madini mkazi wa wilaya ya Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi alisema kuwa zaidi ya watu sita walivamia eneo hilo la mto kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kinyume cha taratibu, kutokana na kutokuwa na vibali vilivyowaruhusu kufanya shughuli hiyo ya uchimbaji katika eneo hilo.


Taarifa hiyo ilieleza kwamba shughuli za uchimbaji wa madini hayo ndani ya mto Muhuwesi zilisimamishwa tangu mwaka 2014 kufuatia pingamizi kutoka kwa Mamlaka ya bonde la mto Ruvuma na bonde la Kusini, kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 na sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004.

Kufuatia taarifa hiyo na baada ya kujionea hali halisi na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na viongozi wao, Waziri Muhongo aliagiza kusitisha haraka shughuli zote za uchimbaji madini kwenye mto huo hadi hapo taarifa ya tathimini ya athari ya shughuli ya uchimbaji kwa mazingira ya mto Muhuwesi itakapokamilika na kuwasilishwa na wataalamu kutoka Mamlaka ya bonde la mto Ruvuma, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).


Ili kuhakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka, Waziri Muhongo alitoa miezi mitatu kwa wataalamu husika kutoka mamlaka hizo wawe wamewasilisha taarifa hiyo kwake na kwa uongozi wa wilaya ya Tunduru tayari kwa kuanza kufanyiwa kazi.

No comments: