Saturday, March 11, 2017

SERIKALI YATAKIWA KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU RAFIKI KWA WATU WENYE ULEMAVU

Martin Mbawala, ambaye ni Mratibu wa mafunzo ya sheria ya watu wenye ulemavu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma akiwasisitiza jambo washiriki wa mafunzo hayo katika kata ya Mpepai wilayani hapa.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

BAADHI ya Watu wenye ulemavu wanaoishi katika kata ya Mpepai Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali izingatie suala la uboreshaji wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa kwenye majengo ya umma yanayoendelea kujengwa hapa nchini kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali.

Washiriki wa mafunzo.
Vilevile wamesisitiza jamii kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu na kwamba wametakiwa kujenga mazoea ya kuwafichua watu wenye tabia ya kuwaficha watoto hao, ili wahusika wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Hayo yalisemwa juzi na Walemavu hao kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa wakichangia hoja mbalimbali katika mafunzo ya siku mbili ya sheria ya watu wenye ulemavu, yaliyofanyika katika kata ya Mpepai halmashauri ya mji huo ambayo yalifadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Foundation for Civil Society.


Akichangia hoja kwenye mafunzo hayo Felix Ndomba mkazi wa kata hiyo alisema kuwa jamii inapaswa pia kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu ikiwemo unyanyasaji, ubaguzi badala yake wanapaswa kujenga mazoea ya kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia ipasavyo kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu.

“Ndugu zangu tunapaswa kuwa wasikilizaji wazuri katika mafunzo haya huko tuendako tukayatumie vyema kwa kufikisha ujumbe huu pia kwa wenzetu ambao hawakubahatika kuhudhuria hapa ili waweze kutambua haki zao za msingi”, alisisitiza Ndomba.

Naye Amos Komba ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya mwanzo wilaya ya Mbinga akitoa mada katika mafunzo hayo, alisisitiza pia mlemavu yeyote yule anatafsiriwa kuwa ni binadamu mwenye haki sawa kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu hivyo anastahili kupata haki zote za msingi kama watu wengine na sio vinginevyo.

Komba alisema kuwa pale mtu mwenye ulemavu anaponyanyaswa kwa namna moja au nyingine, mtu yeyote sheria inamruhusu kutoa malalamiko kwa kamati husika ya maofisa wa ustawi wa jamii au kwenda kushtaki Mahakamani kufungua mashtaka dhidi ya kosa aliloliona linafanyika.

“Kila binadamu amezaliwa hapa duniani kwa ajili ya kuishi kwa hiyo tunapaswa kuthamini utu wa kila mtu, tunapaswa kutambua kwamba mlemavu ni sawa kama alivyokuwa mtu mwingine ambaye hana ulemavu hivyo hatupaswi kuwatenga au kuwabagua”, alisisitiza Komba.


Pia Komba aliongeza kuwa wajibu wa Wizara za serikali hususan kwa ile inayoshughulikia mambo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inapaswa kuhakikisha kwamba, inajumuisha taarifa za miradi inayotekelezwa na wizara hiyo itakayogusa huduma mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu, waandishi, wasanifu majengo na watu wengine wanaojihusisha na ujenzi huo wahakikishe kwamba majengo mapya na viwanja vya michezo vinabadilishwa ili kuwawezesha walemavu wanaingia na kutoka bila kizuizi.    

No comments: