Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo ameeleza kuwa Watendaji
waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo, wametakiwa kuwa tayari
kupokea majukumu yanayoendana na nafasi walizonazo ikiwemo, kasi ya utawala wa
serikali ya awamu ya tano kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Kumbukeni,
vigezo vya Rais wetu John Magufuli anavyovitaka katika nchi yetu ili iweze
kusonga mbele ni kuwa wazalendo kwa mali zetu, kwa manufaa ya wananchi”,
alisema Ndimbo.
|
Askofu John Ndimbo. |
Kadhalika
alibainisha kuwa viongozi wanapopanga mambo ya kimaendeleo, wanapaswa
kushirikisha watu waliopo katika eneo husika na sio kufanya peke yao kwa kukaa
mezani na kutengeneza mambo ambayo siku ya mwisho, yamekuwa yakileta kero na kuzua
migogoro isiyokuwa na tija.
Askofu
Ndimbo alieleza hayo jana alipokuwa akihutubia kwenye kikao cha baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, lililofanyika mjini hapa katika
ukumbi wa Umati huku akiongeza kuwa kiongozi ambaye hatimizi majukumu yake
ipasavyo, anapaswa kujiondoa mapema kabla ya kutokea madhara kwa watu
anaowatawala.
Pia
alitolea mfano kwa kueleza kwamba, kuna baadhi ya watendaji wa vijiji na kata
ambao wamepewa dhamana ya kuongoza wananchi katika maeneo yao wamekuwa
hawatekelezi na kufuata taratibu za nchi kama zinavyotaka, hivyo alishauri
wachukuliwe hatua mapema ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.