|
Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Martin
Msuha akizungumza na wananchi wa kata ya Maguu na Mbuji juu ya mpango wa
serikali unaowataka wakubali kupima maeneo yao ili waweze kuwa na hati miliki
na kuweza kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii, Msuha
alikuwa katika ziara yake ya kikazi ya kuwatembelea wananchi wa jimbo hilo kwa
lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo. (Picha na
Kassian Nyandindi)
|
Na Kassian Nyandindi,
NOVEMBA 5 mwaka jana Rais Dkt. John Magufuli ametimiza mwaka
mmoja tangu aingie madarakani, alipochaguliwa kushika wadhifa huo baada ya
uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 ambao pia ulivishirikisha vyama
mbalimbali vya upinzani.
Kama inavyofahamika wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu
uliopita Rais huyo aliahidi masuala ambayo angeyatekeleza mara tu baada ya
Watanzania kukipatia ridhaa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuongoza nchi, ambapo
mpaka anatimiza mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani amefanikiwa kutimiza
ahadi zake kwa asilimia kubwa na hivyo kuwafanya wananchi kuendelea kujenga
imani kwa kiongozi huyo.
Wakati Watanzania hao wakishuhudia utendaji kazi wa kizalendo
ambao umekuwa ukiendelea kutekelezwa na Dkt. Magufuli, Wabunge nao kwa upande
wao wanapaswa kujitathimini na kueleza nini hasa wamewafanyia wananchi
wao waliowachagua tangu walipoingia madarakani mara baada ya uchaguzi
mkuu kufanyika Oktoba 25 mwaka 2015.
Ikumbukwe kwamba ushindi huo wa CCM ulitokana na Watanzania
hawa kuwa na imani kubwa na chama hicho, hivyo kinachotakiwa sasa kwa viongozi
wake ni kuendelea kutekeleza kwa vitendo yale yote ambayo yameainishwa ndani ya
Ilani ya uchaguzi huo sambamba na yale ambayo waliahidi wao binafsi.
Katika uchaguzi huo mkuu ambao wabunge, madiwani na
Rais walichaguliwa zipo pia ahadi mbalimbali zilitolewa kwa madai kwamba
wangezitekeleza mara tu wakichaguliwa na kuingia madarakani, sasa ni vyema kila
baada ya kipindi fulani viongozi hao ni muhimu wakayatafakari yale yote ambayo
wameyafanya ili wananchi waweze kuyafahamu.
Katika makala haya, mmoja kati ya Wabunge ambao walitoa ahadi
kwa wananchi wakati wa kuomba ridhaa ya kushika nafasi hiyo ya uwakilishi wa
kuongoza wananchi, Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Martin
Msuha ambaye alipeperusha bendera ya CCM na kuonekana kuwa mshindi katika
kinyang’anyiro hicho mara baada ya uchaguzi huo kufanyika.