|
Wagonjwa wanaodaiwa kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na sumu wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Mji wa Mbinga. |
|
Baadhi ya Wahudumu wa afya katika hospitali ya Mji wa Mbinga wakiendelea kuwahudumia wagonjwa jana ambao wanadaiwa kunywa kinywaji kinachodaiwa kuwa sumu aina ya togwa, ambacho hata hivyo hali za wagonjwa hao zinaendelea vizuri baada ya kuwahi matibabu katika hospitali hiyo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATU 72 ambao ni Wakazi wa kitongoji
cha Kipika kata ya Matarawe katika Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamenusurika
kupoteza maisha baada ya kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na
sumu.
Aidha imeelezwa kuwa tukio hilo
lilitokea Novemba 19 mwaka huu majira ya mchana, ambapo kinywaji hicho
walikunywa wakiwa kwenye sherehe (Harusi) iliyokuwa ikifanyika katika kitongoji
hicho.
Mmoja kati ya wagonjwa waliolazwa
katika wodi ya wanaume hospitalini hapo, Chirwa Mohamed Hassan akizungumza na
mwandishi wetu alisema kuwa baada ya kunywa kinywaji hicho na masaa machache
kupita, ghafla yeye na wenzake walijikuta tumbo linauma na kuanza kuharisha
mfululizo ndipo walikimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.
“Baada ya kula chakula tulipewa togwa
tulikuwa tunakunywa masaa machache yalipopita ndipo tumbo lilianza kuuma na
kuharisha lakini baada ya kuwahi hapa hospitalini, tunawashukuru waganga kwa
kutupatia matibabu kwa uharaka na sasa tunajisikia kuna unafuu kidogo”, alisema
Hassan.