Thursday, April 11, 2013

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUVAMIWA NA TEMBO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Daraja mbili kata ya Namwinyu tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Chalamanda  Masapi (65) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na Tembo.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa marehemu Masapi  alikumbwa na mkasa huo  baada ya kukutana na tembo huyo ambaye alikuwa na mtoto, ghafla wakati akikagua uharibifu wa mazao uliofanywa na kundi la wanyama hao, katika shamba lake lililopo nje kidogo na kijiji hicho.

Mtoto wa marehemu Chalamanda ambaye alikuwa ni miongoni mwa shuhuda wa tukio hilo Rashid Chalamanda  alisema, yeye na marehemu baba yake kwakushirikiana na kundi la wananchi wanaolima katika eneo hilo, walikwenda katika mashamba yao kushiriki katika zoezi la kuwafukuza tembo hao ambao pia walivamia kijijini hapo na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao yao.


Alisema katika tukio hilo la kushitukiza marehemu  alijikuta akiwa mikononi mwa mnyama huyo,  ambaye baada ya kumkamata kwa kutumia mkonga wake  alimrusha juu na kukinga katika mti uliokuwa karibu na eneo hilo, kabla ya kumkanyaga na kumsaga na baadae kumpiga kwa kutumia pembe zake na kumtoboa toboa vibaya mbavuni na tumboni.

Akizungumzia tukio hilo afisa wanyama pori wa wilaya hiyo Peter Mtani pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo, alisema kuwa tayari idara yake imepeleka askari wenye silaha ili waende kuandaa mtego, ambao utafanikisha kuuawa kwa tembo huyo.

Mtani aliendelea kueleza kuwa  matukio ya tembo hao kuvamia na kufanya uharibifu katika mashamba ya wakulima wa Tunduru, yamekuwaa yakijitokeza mara kwa mara na kwamba kutokana na hali hiyo idara yake imekuwa ikifanya kazi ya ziada kuwafukuza wanyama hao,  ili wasiendelee kuharibu mazao ya watu.

Alisema pindi inapobainika kuwa tembo hao wanazidi kufanya mashambulizi ya kuua watu idara hiyo pia imekuwa ikichukua hatua za kuwasaka na kuwaua tembo hao haraka iwezekanavyo  ili wasiweze kusababisha madhara kwa watu wengine.

Akizungumzia hali na muonekano wa mwili wa marehemu huyo mmoja kati ya waganga wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dkt.  George Chiwangu alisema kuwa marehemu alifariki dunia kutokana na kutokwa na damu nyingi zilizosababishwa na kutobolewa matundu manne ubavuni na tumboni.

Dkt.George Chiwangu aliendelea kueleza kuwa  sambamba na hali hiyo pia mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umevurugika vibaya huku shingo yake ikiwa imevunjika na kichwa kupasuka.

No comments: