Monday, April 15, 2013

BREAKING NEWS: MVUA YASABABISHA MAAFA WILAYANI NYASA, MAKAZI YA JAA MAJI, MTU MMOJA AFARIKI DUNIA NA EKARI 45 ZA SOMBWA NA MAJI

Ziwa Nyasa.


















Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

YAMEJITOKEZA maafa makubwa  wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo, na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia, mazao yaliyolimwa shambani na mifugo kusombwa na maji.

Tukio hilo limetokea usiku wa tarehe 14 mwaka huu, ambapo watu wamekosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kujaa maji na kulazimika, kwenda kuomba msaada kwa majirani wenzao.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi alisema kunyesha kwa mvua hizo kumesababisha kuwepo kwa maji mengi yaliyokuwa yakitokea milimani na kuelekea kwenye makazi ya watu.


Kahindi alivitaja vijiji vilivyoathiriwa kutokana na maafa hayo ni Mbamba bay, Kilosa, Ngindo, Lundo na kwamba mtu aliyefariki ni mkazi wa kijiji cha Ndengele anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 55, ambapo alikutwa na mauti wakati akitokea mtoni kuchota maji na jina lake bado halijafahamika.

Vilevile alieleza kuwa hali hiyo imesababisha ekari 45 za wananchi, zilizolimwa mazao ya mihogo na mpunga zimesombwa na maji ikiwemo na skimu ya Kimbande ya kilimo cha umwagiliaji zao la mpunga.

Katika skimu hiyo mabanio mawili ya kuhifadhi maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, yamebomoka na kusombwa na maji ikiwemo na mifereji yake ya kupeleka maji shambani.

“Mifugo iliyozolewa na maji na kufa ni ng’ombe tu, na sasa wamefikia idadi yake wapo saba, hivyo tunaendelea kufanya tathimini na uchunguzi zaidi taarifa kamili ya hata idadi nyumba zilizoathiriwa itatolewa baadaye”, alisema Kahindi.

Kadhalika alisema madaraja manne yaliyojengwa katika vijiji vya Lipingo, Liuli, Lundo na Ndengele yamezolewa na maji na kusababisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo, kukosa mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Timu ya wataalamu ya wilaya ya Nyasa kwa kushirikiana na wilaya mama ya Mbinga, wamekwenda huko kwa ajili ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kuokoa na kusaidia huduma muhimu kwa watu walioathirika.

Hadi sasa hali ya uokoaji inaendelea vizuri kutokana na maji kupungua, lakini kumegundulika mnyama mkali aina ya mamba akizagaa nchi kavu katika eneo la Mbamba bay mjini, ambapo timu ya wataalamu wa maliasili wamekwenda huko kwa ajili ya kumuua ili asiweze kuleta madhara katika jamii.

No comments: