Tuesday, April 9, 2013

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AOMBWA KUINGILIA KATI SUALA LA KUINUA KIWANGO CHA MPIRA WA MIGUU NA MIKONO MBINGA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.




















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WADAU wa michezo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamemuomba Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, kuingilia kati suala la kuinua kiwango cha mpira wa miguu na mikono wilayani humo.

Vilevile wadau hao walisema endapo mkuu huyo wa wilaya atafanya hivyo, wana hakika kiwango cha mpira wilayani humo kitaenda vizuri, na kuifanya wilaya hiyo wananchi wake waweze kupenda michezo.

Hayo yalisemwa na wadau hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu, kwa nyakati tofauti mjini hapa.


Walishauri pia, katika kila msimu wa mavuno ya kahawa ni vyema ukaanzishwa utaratibu kwa wafanyabiashara wanaonunua zao hilo kuchangia kiasi kidogo cha fedha kwa kila kilo moja ya kahawa, ili fedha hizo ziweze kutumika katika kuendeshea shughuli za mpira wa miguu kipindi ligi mbalimbali zinapoendeshwa.

Walieleza kuwa suala hilo ni vyema lifikishwe kwenye vikao husika vya halmashauri ya wilaya hiyo ikiwemo Baraza la madiwani ili waweze kutoa baraka zao na kuweka mikakati madhubuti ya kuweza kufanikiwa suala hilo.

Kadhalika walieleza kuwa endapo suala hilo litabarikiwa katika vikao hivyo, halmashauri ianzishe akaunti maalum ya michezo ambayo itasimamia na kuweza kusaidia vilabu vya mpira wa miguu na mikono viweze kusonga mbele.

Vilevile waliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo, itasaidia kuvifanya vilabu vya mpira kutokuwa ombaomba na hatimaye kujiendesha vyenyewe.






No comments: