Friday, April 19, 2013

WATUMISHI WAZEMBE KAZINI TUNDURU, KUFUKUZWA KAZI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.


















Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya wilaya hiyo, kuwachukua hatua ikibidi hata kuwafukuza kazi, watumishi wasiowajibika ikiwa ni juhudi za serikali kuinua taaluma wilayani humo.

Nalicho alisema hayo wakati akifunga mkutano wa kutathimini matokeo kidato cha pili, nne na sita uliofanyika katika ukumbi wa klasta Mjini humo na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na serikali kubaini kuwa watumishi  wa kada zote wilayani humo, hawako tayari kufanya kazi kwa kujituma hali iliyopelekea wilaya hiyo kuwa nyuma kielimu.

 “Viongozi ndio wasiopenda kufanya kazi, wamebakia kula mishahara tu na ndiyo maana katika wilaya hii, tumeendelea kuwa nyuma kielimu”, alisema Nalicho na kuongeza kwa kumtaka mkurugenzi awachukulie hatua za kinidhamu.

Alisema inashangaza kuona kuwa Tunduru ikiwa imekithiri kwa utoro wa wanafunzi lakini inapotokea ofisi yake inahitaji taarifa za matukio hayo maafisa tarafa, watendaji wa kata na viongozi wa vijiji wengi wanapoulizwa juu ya idadi ya wanafunzi waliofaulu na kucahaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari wanadai kutokuwa na takwimu zake.

Nalicho aliendelea kubainisha viashiria vingine vya viongozi hao kutowajibika kuwa ni pamoja na kuwepo kwa takwimu kubwa za utoro  ambazo hazifanyiwi kazi, amnapo alitolea mfano shule ya msingi Njenga ambayo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2010 ilifaulisha wanafunzi 41 waliokwenda shule walikuwa 3 mwaka 2011 walifaulu 46 walioendelea na masomo 7 na mwaka 2012 walifaulu 17 waliokwenda shule hadi sasa 1.

Naye Mwenyekiti wa huduma za jamii Diwani Athumani Nkinde pamoja na kukiri kuwa zipo shule za sekondari ambazo zilijengwa kisiasa na kutolea mfano shule ya sekondari Nampungu, ambayo inaonesha kutelekezwa na wananchi kwa kutopeleka wanafunzi alipigilia msumali wa moto kwa kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria, kwa wanafunzi na wazazi wao ambao hawakupeleka watoto katrika shule hiyo.

Akizungumzia mikakati ya kuinua taaluma na kuiondoa idara yake katika kashfa hii ya kupeleka sekondari wanafunzi wasiojua kuandika, kusoma na kuhesabu kaimu afisa elimu wa shule za msingi Flavian Nchimbi alisema kuwa wilaya inaendelea kujidhatiti kwa kutumia mitihani ya majaribio katika kata pamoja na kuendesha mafunzo ya mada ngumu kwa walimu ikiwa ni juhudi ya kuinua taaluma kwa wanafunzi hao.





No comments: