Tuesday, April 30, 2013

MWALIMU MSTAAFU AFARIKI DUNIA KWA KUNYWA GONGO

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki




















Na Steven Augustino,
Tunduru.

MWALIMU mstaafu katika kijiji cha Kidodoma wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma Rajab Mohamed Kalesi (65) amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kunywa pombe haramu ya gongo.

Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mdogo wa marehemu  Athuman Saidi walisema kuwa kabla ya mkasa huo, marehemu huyo alionekana akinywa Pombe hiyo kwa siku mbili mfululizo, huku akiwa amejificha katika nyumba ya muuzaji wa pombe hiyo Hamdi Swalehe.

Habari zinaeleza kuwa mwalimu huyo kabla ya kukutwa na mauti, alikuwa akiwa anatamba kuwa na fedha nyingi, alizokuwa ametoka kulipwa kama mafao ya kustaafu kazi hiyo.


Walisema kufutia taarifa hiyo ya kupokea fedha  hizo anadaiwa kuwa na fedha zaidi ya shilingi milioni 48, alionekana kutembea na wapambe muda wote huku wakienda kujipatia kinywaji hicho kwa wingi, na kumsababishia kupoteza uhai wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Nampungu Rehema Nyoni na mtendaji wa kijiji hicho, Mbuyu Allky Mbuyu walisema kuwa baada ya wapambe wake kuona hali ya mwalimu huyo inabadilika walitokomea kusikojulikana, na kumuacha peke yake katika nyumba ya muuza pombe hiyo hadi mauti yalipomkuta.

Walisema akiwa katika hali ya kutapatapa mke wa muuza pombe alijitahidi kuokoa maisha yake kwa kumpatia huduma ya kwanza kwa kumpepea, na kumwagia maji ya baridi huku akimnywesha uji, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na alipokata roho mumewe 

Hassani Swalehe alitimua mbio na kumwacha marehemu akiwa peke yake.
Akizungumzia tukio hilo mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo Dokta Goerge Chiwangu alisema, chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na unywaji wa pombe nyingi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo, na kuongeza kuwa jeshi la polisi linamshikilia mke wa muuza pombe hiyo haramu, ambaye hakumtaja jina lake kwa ajili ya uchunguzi.

No comments: