Tuesday, April 30, 2013

GODBLESS LEMA ALIA NA POLISI, ASIMULIA JINSI WALIVYOMVAMIA NYUMBANI KWAKE

Umati wa watu ukiwa umejaa nje ya jengo la Mahakama Arusha, kusikiliza kesi ya Lema.



















Na Waandishi wetu,
Arusha.

MBUNGE wa Arusha mjini Godbless Lema kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambaye amechiwa huru kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa huo, amewataka wanachama wa chama hicho kumzomea mkuu wa mkoa wa Arusha Magessa Mulongo kila watakapomuona.

Pia Lema amesimulia jinsi alivyovamiwa nyumbani kwake, usiku wa kuamkia Aprili 26, mwaka huu.

Lema akiwa amefuatana na wafuasi na wanachama wa Chadema walikusanyika katika viwanja vya Ngarenaro ambako mbunge huyo aliwahutubia kwa dakika kadhaa na kuwataka wafuasi wake warejee nyumbani.

Awali wakati wanachama na wafuasi wa chama hicho wakiandamana, walisikika wakiimba; Lema mwamba, Lema jembe, Lema, Lema ni chaguo la Mungu Arusha!

Hayo yalikuwa ni baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwenye umati wa wafuasi, wapenzi na wanachama wa chama hicho  kutoka Arusha mjini.


Mbunge huyo akizungumzia jinsi polisi walivyovamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Aprili 26 mwaka huu, alisema awali alijua kwamba watu waliokuwa wamezunguka nje ya nyumba yake walikuwa ‘wang’oa kucha’ lakini kumbe haikuwa hivyo.


Awali Lema anasema kwamba alifikiri kwamba wameenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumng’oa kucha baada ya kushuhudia baadhi yao wakiruka ukuta na wengine wakiingia ndani wakimshawishi  ajisalimishe mwenyewe.

Mbali na simulizi hiyo pia Lema alimshukuru na kumsifia mke wake, Neema kwa ujasiri aliouonyesha baada ya kuamua kuzungumza na askari ambao awali waliojitambulisha kuwa ni polisi.


Moja ya mambo ambayo Neema alizungumza na polisi ni kwamba walimuamuru awaonyeshe mahali aliko mbunge huyo, lakini mke wake Lema aliwataka polisi hao wamuonyeshe kibali cha kumkamata mbunge huyo kutoka ofisi ya Spika wa bunge au hati kutoka polisi.


“Mambo yalikuwa hivyo, watu hao waliokuwa wameelekeza mitutu ya bunduki chumbani kwangu na walianza kuhesabu wakitishia kufyatua risasi na kulipua mabomu nisipojisalimisha. 

Hapa nilihofia maisha ya mke wangu na watoto wangu kikiwamo kichanga cha miezi sita kiasi cha kufikiria kwamba bora nife mimi na watoto na mke wangu  wasalimike,” amesema Lema.

Hivi msemo wa ‘wang’oa kucha’ umenea kwa kasi nchini kutokana na kuwapo kwa matukio ya kutekwa na kuteswa kwa watu mbalimbali nchini. 


Mmoja wa tu waliotekwa, kuteswa na kung’olewa kucha ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Steven Ulimboka.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema kuanzia Alhamisi wiki hii, chama hicho kitafanya mikutano ya hadhara katika Kata za Ngarenaro na Sombetini kunadi sera na kujiimarisha kwa wananchi.


Lema anakabiliwa na kesi ya kutoa maneno ya uchochezi iliyosomwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi ya mkoa wa Arusha.
 

No comments: