Friday, April 12, 2013

BREAKING NEWS: WAANDISHI WAWILI NA AFISA UHAMIAJI WAFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI MKOANI TANGA

IGP Said Mwema























Na Mwandishi wetu,
Tanga.

AJALI mbaya iliyotokea jana wilaya ya Handeni mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu watatu, ambao ni waandishi wa habari wawili kutoka kampuni ya Mwananchi Communication na gazeti la Uhuru na Mzalendo, Radio Aboud na Ofisa Uhamiaji wa wilaya hiyo.
 
Ajali hiyo iliyotokea Aprili 11 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi iliuhusisha msafara wa Mkuu wa wilaya hiyo Muhingo Rweyemamu, ni msafara unaodaiwa kuwa ulikuwa na magari matatu tu lakini gari moja liliacha njia na kupinduka.

Waliofariki ni pamoja na Hussein Semdoe mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Hamis Bwanga wa Radio Uhuru na Abood pamoja na Mariam Hassan ambaye ni Ofisa Uhamiaji wilaya ya Handeni.

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo pamoja na vifo vya marehemu hao.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Mkuu wa wilaya hiyo alisema ajali hiyo ilitokea wakiwa kwenye msafara, kuelekea Ndolwa kupanda miti.

Muhingo alieleza kwamba gari lililopata ajali ni la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, lenye namba za usajili STJ 4673 ambalo ndilo lililokuwa likitumiwa na Ofisa Uhamiaji, Hassan pamoja na wanahabari hao.

Alisema huu ni msiba  mkubwa kwa wilaya ya Handeni kwani wamepoteza wachapakazi na watu muhimu katika mchakato wa maendeleo ya wilaya hiyo.

"Wilaya ya Handeni imepoteza wanahabari kwa asilimia 100, kwani waandishi hawa ndiyo walikuwa wanahabari pekee wilayani hapa,

"Msiba huu ni mkubwa si kwa tasnia ya wanahabari pekee bali hata kwa juhudi za maendeleo ya wilaya ya Handeni, tulikuwa tukizunguka nao katika shughuli mbalimbali hapa wilayani hivyo ni pigo kubwa," alisema Muhingo.
 
Aidha Mkuu wa wilaya hiyo alisema marehemu Hassan ambaye alikuwa afisa uhamiaji kabla ya umauti alikuwa mpambanaji mkubwa wa wahamiaji haramu katika wilaya hiyo.

Aliongeza kuwa hivi karibuni alifanikiwa kuwakamata takribani wahamiaji 70 eneo hilo, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa nguvu kazi ya wilaya ya Handeni.

Miili ya waandishi imechukuliwa na ndugu na kwamba serikali inatoa pole kwa ndugu na jamaa waliopatwa na matatizo hayo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga Costantine Massawe amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.

No comments: