Friday, April 19, 2013

TUNDURU SEKTA YA ELIMU BADO NI TATIZO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEBAINISHWA kuwa mahusiano mabaya kati ya Walimu na Wanafunzi ni moja kati ya kikwazo kilichoelezwa kwamba huchangia kuzorota kwa elimu wilayani humo.

Kadhalika  wanafunzi kukataa kukaa katika mabweni au hosteli ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya elimu wilayani Tunduru na kusababisha wilaya hiyo kupata matokeo mabaya kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha pili na nne katika kipindi cha mwaka 2011/2012.

Hayo yalibainishwa na afisa elimu sekondari Ally Mtamila wakati akiwasilisha taarifa yake ya matokeo ya kidato cha pili na cha nne katika kipindi cha mwaka 2011/2012 katika mkutano maalum ulioketi wilayani humo, na kuongeza kwa kuwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika usimamiaji wa watoto wao ili waweze kuwa na hamasa ya kupenda masomo wanapokuwa shuleni au nyumbani.


Vilevile wazazi kukemea watoto wanaokwepa kuingia darasani ambao wamekuwa wakiachwa waendelee kucheza wakati wenzao wakiwa darasani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mwaka 2011 matokeo ya kidato cha pili wilaya hiyo ilifaulisha kwa wastani wa asilimia 35%, huku takwimu hizo kwa upande wa matokeo ya kidato cha nne katika kipindi cha mwaka 2012 zikionesha kuwa wilaya, ilifaulisha kwa wastani wa asilimia 59.46% kiwango kilichodaiwa kuwa ni kidogo na kiliifanya kushika nafasi ya mwisho kimkoa.

Awali akifungua mkutano mkuu wa wilaya ya Tunduru  Chande Nalicho pamoja na kubainisha kuwa serikali kuwa na vipaumbele vingine vya maendeleo lakini elimu ni muhimu kwa kile alichoeleza kwamba ndio msingi wa maisha.

Nalicho alieleza kuwa ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Tunduru, ni lazima wilaya ijikite katika kusimamia elimu kwanza mambo mengine yafuate baadaye.

Katika taarifa hiyo mkuu huyo wa wilaya, alitolea mfano wa takwimu za ufaulu wanafunzi 2764 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari  hadi mwishoni mwa mwezi wa tatu, ni asilimia 60% ya  watoto wote waliochaguliwa  kujiunga na masomo ya sekondari.

Akizungumzia upande wa shule za msingi  mwaka 2011shule ya msingi Nakapanya wilayani humo, ilifaulisha watoto 26 lakini takwimu zinaonesha kuwa  watoto wote hawakwenda shule na kuongeza kuwa, hali hiyo inawakatisha tamaa walimu wa shule za msingi zinazoendele kufaulisha watoto.  

Wakichangia kwa nyakati tofauti mwalimu Issa Ngajime alisema kuwa chanzo cha kushamiri kwa utoro, uchangiaji hafifu wa chakula mashuleni na wanafunzi kukataa kukaa katika hostel zilizojengwa katika shule zao, viongozi wa serikali za vijiji wanastahili kubeba lawama, huku wakiwataka viongozi kutochanganya elimu na siasa.

Aidha mbinu za kufundishia imeshauriwa kuendelea kuboresha na kuchukua hatua kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakibainika kuchaguliwa wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mkuu wa shule ya Mgomba Elis Banda alisema kuwa tatizo la wanafunzi kukataa kukaa katika hosteli, linatokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaosoma katika shule hizo kuwa ni wakazi wa maeneo husika na akapendekekeza kuwepo kwa utaratibu wa kutenga shule za kanda kwa ajili ya kupeleka wanafunzi kutoka maeneo tofauti, huku akiitaka serikali kutoa maelekezo ya vitabu vya kununua tofauti na sasa ambapo kumekuwa na maelekezo ya kuwataka wakuu wa shule kutumia vitabu kutoka katika kampuni ya EMACK.

Wanafunzi kupewa mamba imekuwa nalko ni tatizo lakini bodi za shule zimekuwa zikifanya kazi ya ziada kudhibiti hili, lakini kila wanapofuatilia matokeo ya kesi polisi huwa
hawapatiwi majibu ya maendeleo ya kesi husika hali inayo wakosesha imani kuwa huenda kesi hizo zimekuwa zikipeleka ulaji kwa jeshi hilo.

Mkuu wa shule ya sekondari Lukumbule Mathias Katto akabainisha vikwazo vingine kuwa shule zao kutokuwa na walimu wa masomo ya Sayansi, kutokuwa na maktaba na nyumba za walimu kutokuwa bora ni kikwazo kimojawapo.

Marafiki hao wa elimu pia wakanyooshea kidole mila na desturi potofu za kuwafundisha watoto wadogo, hasa wakike mafunzo ya kuishi kinyumba ambayo hutolewa kupitia mafunzo  katika jando, Unyago na Msondo na ngoma ya Sakamimba hali ambayo imekuwa ikipelekea baadhi ya wanafunzi, kuishi kwa wanaume huku wakiwa wanaendelea na masomo.

No comments: