Thursday, April 11, 2013

VIKONGWE WAKAMATWA WAKIWAFUNDISHA WATOTO USHIRIKINA, WASWEKA RUMANDE KULINDA USALAMA WAO

Na Steven Augustino,

Tunduru.

VIKONGWE wa tano kutoka katika kijiji cha Mtonya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamezuiliwa katika kituo kidogo cha polisi Nakapanya, ili kulinda usalama wa maisha yao na kuwafanya wasishambuliwe kutokana na kutuhumiwa kufanya ushirikina na kuwafundisha taaluma hiyo watoto wa watu bila ridhaa ya wazazi wao.

Tukio hilo lilitokea baada ya vikongwe hao wanaodaiwa kuwa na uwezo wa kufungua na kuingia katika nyumba za watu kwa njia za kishirikina, walifumwa wakifanya vitendo hivyo katika kijiji cha Mindu wilayani humo.

Taarifa zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nakapanya Kubodola Ambali, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Spia Msusa (50), Ayana Iddi (75) Adresia Maulid (68), Jenifer Saimon(60) na mwingine aliyefahamika kwa jina la Biti Nyoya mwenye umri wa miaka 60.


Ambali alifafanua kuwa mpango huo uligundulika baada ya wazazi wa mtoto Ally Milongo, kuamka na kuanza kumtafuta mtoto wao mwenye umri wa miaka 10 kutoweka usiku wa manane katika mazingira ya kutatanisha, ndani ya nyumba yao.

Baba wa mtoto huyo Milongo Ally alisema kuwa baada ya tukio hilo la kutoweka kwa mtoto wake, yeye na mkewe waliamka na kuanza kumtafuta katika maeneo tofauti ya kijiji hicho, ambapo baadaye wakafanikiwa kuwaona wazee hao wakiwa uchi wa mnyama pamoja na kijana wao, na walipojaribu kuwasogelea vikongwe hao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema baada ya tukio hilo walimkamata mtoto wao na kwenda naye nyumbani kwao, na baada ya kumbana na kumtaka aeleze alikokuwa ndipo akawataja watu hao ambao baada ya kuitwa walikiri na kuomba radhi kuwa hawatarudia tena, kumchukua mtoto huyo ambaye walidai kuwa ni miongoni mwa washirika wao wa muda mrefu.

Alisema katika tukio hilo wazee hao walitozwa faini ya shilingi 100,000 ambayo waliilipa papo hapo, na baadae wakaruhusiwa kuondoka.

Akiongelea tukio hilo mtoto Ally Milongo alisema kuwa wakiwa  mara kwa mara na washirikina hao wamekuwa wakienda kumchukua yeye na watoto wenzake wane, na kuwapeleka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwafundisha utaalamu kuingia na kuwachezea watu nyakati za usiku, na baadae hurejea majumbani kwao na kufungua milango kwa kutumia matako huku wazazi wao wakiwa hawafahamu kinachoendelea.


No comments: