Friday, May 1, 2015

WANANCHI TUNDURU WATAKIWA KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA MPIGA KURA

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akijiandikisha katika uzinduzi wa uandikishaji wa kitambulisho cha taifa katika kituo kilichopo kwenye ofisi za Mkuu huyo wa wilaya wilayani humo, kushoto kwake ni Afisa wa NIDA wilayani Tunduru. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewahimiza wananchi wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kupata vitambulisho vya kitaifa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo ambalo lilifanyika kwenye ofisi za mkuu huyo wa wilaya, zilizopo mjini hapa.

Nalicho alifafanua kuwa miongoni mwa faida za vitambulisho hivyo, ni pamoja na kila Mtanzania kutambuliwa kadhalika kitakuwa na msaada mkubwa kwa mtu binafsi hasa pale anaposafiri nje ya nchi.

Alisema kuwa wito huo ameutoa kwa wananchi wake wa wilaya hiyo, kutokana na kuwa pembezoni mpakani mwa Tanzania na Msumbiji hivyo kuwepo kwa vitambulisho hivyo kutasaidia hata mamlaka husika, kuwatofautisha wananchi wake kutokana na muingiliano uliopo miongoni mwao.

Thursday, April 30, 2015

MBIO ZA MWENGE RUVUMA KUZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 10.3

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Alli Mohamed Shein akikabidhi Mwenge wa uhuru kwa mmoja wa wakimbiza Mwenge kitaifa, jana mara baada ya kuzindua mbio hizo katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akikabidhi Mwenge wa uhuru kwa Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani humo, Profesa Norman Sigalla kwa ajili ya kuanza mbio zake katika wilaya ya Songea.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dokta Alli Mohamed Shein amekemea kitendo kinachofanywa na baadhi ya watu kuwagawa Watanzania, jambo ambalo linahatarisha amani ya nchi yetu.

Dokta Shein alisema kumekuwa na makundi ambayo huwagawa kwa misingi ya dini, rangi na ukabila jambo ambalo amekemea vikali na kutaka hali hiyo iachwe mara moja.

Vilevile alikemea vitendo vya biashara ya madawa ya kulevya, ambapo alieleza kuwa kundi la vijana ndilo kwa kiasi kikubwa linahusika na vitendo hivyo na kuwataka waachane na tabia hiyo badala yake wafanye shughuli za kimaendeleo, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Rais huyo alifafanua kuwa ni aibu kwa taifa hili vijana kujihusisha na biashara hiyo, kwani wao ndio nguvu kazi katika kusukuma gurudumu la maendeleo hivyo serikali itaendelea kupambana na vitendo hivyo vya uuzaji wa madawa hayo, ili visiweze kuendelea.

OFISA USALAMA WA TAIFA ALETA KIZAZAA KWENYE UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU KITAIFA RUVUMA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dokta Fenera Mukangara kushoto akimuongoza Rais wa Zanzibar Dokta  Alli Mohamed Shein, kwenda kuzindua mbio za Mwenge wa uhuru jana, katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma. (Picha na Muhidin Amri)
Na Mwandishi wetu,
Songea.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Waandishi wa habari mkoani Ruvuma jana wamejikuta wakifanya kazi katika mazingira mgumu, baada ya mmoja wa Ofisa kutoka idara ya usalama wa taifa hapa nchini, kuwazuia waandishi hao wasitekeleze majukumu yao ya kazi ipasavyo.  

Ofisa usalama huyo aliwazuia wasiweze kupiga picha, na kuandika taarifa za uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa, zilizofanyika jana kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Aidha aliwashangaza waandishi hao pale alipofikia hatua ya kutamka kwamba wasitekeleze majukumu yao ya kazi, mpaka mgeni rasmi Dokta Alli Mohamed Shein atakapokwenda kuketi jukwaani jambo ambalo wanahabari hao walimpuuza na kutumia mbinu mbadala katika kuandika habari, na kupiga picha za tukio hilo.

MWAMBUNGU ATAKA WANANCHI WA KITONGOJI CHA MANGAWAGA NYASA WASIHAMISHWE

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ametoa agizo la kuutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani humo, kusitisha mara moja mchakato wa kuwahamisha wakazi wa kitongoji cha Mangawaga kijiji cha Mkalole kata ya Kilosa wilayani humo, mpaka serikali itakapotoa maelekezo mengine.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa mkoa, liliwasilishwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.

“Ndugu zangu nimeagizwa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ni marufuku kuhama endeleeni kuishi hapa kijijini mpaka serikali itakapotoa maelekezo mengine, hivyo ondoeni wasiwasi katika jambo hili ninalowaambia”, alisema Njowoka.

DEREVA WA PIKIPIKI MBINGA APANDISHWA KIZIMBANI KWA KULAWITI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

LAURENT Kibasa (30) ambaye ni dereva wa pikipiki, mkazi wa mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya hiyo, kwa tuhuma ya kumlawiti mwanaume mwenzake (Jina tunalo) mwenye umri wa miaka 24 na kumdhuru mwili.

Mwendesha mashtaka msaidizi wa polisi, Inspekta Seif Kilugwe alidai mbele ya Hakimu Joachimu Mwakyolo wa Mahakama ya wilaya ya Mbinga, kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 23 mwaka huu majira ya mchana akiwa nyumbani kwake baada kushindwa kulipwa deni analodai shilingi 85,000.

Kibasa anadaiwa kufanya makosa hayo kwa dereva wa pikipiki mwenzake maarufu kwa jina la Boda boda, baada ya kumfuata kwenye eneo lake la kazi kisha kumkamata na kumpeleka nyumbani kwake ambako anadaiwa alimfunga kamba mikononi na kuanza kumpiga, kwa kutumia mkanda wake wa suruali.

Tuesday, April 21, 2015

SERIKALI YATAKIWA KUTOA KIBALI KWA TAASISI BINAFSI KUSAMBAZA RASIMU YA PILI YA KATIBA

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

SERIKALI hapa nchini, imetakiwa kutoa kibali kwa taasisi binafsi ziweze kushiriki kikamilifu kuchapisha nakala za rasimu ya pili ya katiba inayopendekezwa, ili zisambazwe kwa wingi na kumfikia kila mwananchi kwa wakati, hatimaye waweze kuisoma na kuielewa na baadaye waipigie kura ya maoni wakiwa na taarifa sahihi.

Hayo yalisemwa na mtafiti wa maswala ya katiba hapa nchini, Gelin Fuko kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu wakati alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara Mbinga mjini mkoani Ruvuma, uliofanyika kwenye viwanja vya soko kuu mjini humo.

Aidha Fuko aliwataka wananchi wakati utakapofika katika maeneo yao, wajiandikishe kwenye daftari la wapiga kura jambo ambalo litawafanya waweze kuingia kwenye mchakato huo, wa kuipigia kura rasimu hiyo.

Saturday, April 18, 2015

WAFARIKI DUNIA NA WENGINE 20 KUJERUHIWA VIBAYA KATIKA AJALI YA GARI WAKIELEKEA MNADANI

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa vibaya, kufuatia ajali ya gari aina ya Mitsubishi Fuso kupinduka katika kijiji cha Burma wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo kumshinda kona za milima ya Ambrose zilizopo katika kijiji hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema kuwa ajali hiyo, imetokea leo majira ya saa 3:30 asubuhi katika kijiji hicho wilayani humo.

Msikhela alifafanua kuwa gari hilo lilikuwa likitokea Songea kwenda Mbamba bay, wilaya ya Nyasa huku likiwa limebeba watu hao, pamoja na mizigo kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli za mnada.

Friday, April 17, 2015

KAMANDA UVCCM AISAMBARATISHA CHADEMA NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Mbamba bay.

BAADHI ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamekiasi chama hicho na kuhamia Chama Cha Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichoeleza kuwa, wamechoshwa na sera za Chadema ambazo zimekuwa zikichochea machafuko mara kwa mara hapa nchini.

Wafuasi hao ambao walikuwa 67 walieleza kuwa, hawana sababu ya kuendelea kuwa katika chama hicho cha upinzani badala yake waliona ni heri warejee kwenye chama mama, CCM ambako walikuwa tokea awali.

Hali hiyo ilitokea leo katika viwanja vya mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo, kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa, Cassian Njowoka.

Thursday, April 16, 2015

AWEZAE AFARIKI DUNIA KWA KUGONGWA NA LORI TUNDURU

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

AWEZAE Mohamed (35) amefariki dunia kufuatia ajali mbaya iliyotokana na pikipiki ambayo alikuwa akisafiria, kugongwa na lori aina ya Steya lenye namba za usajili T 862BFW ambalo linatumiwa kubeba kifusi cha udongo.

Kadhalika mume wake Issa Swalehe naye amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru kufuatia ajali hiyo, ambaye ni mlinzi katika kampuni ya kichina ambayo inajenga barabara kutoka Tunduru mjini hadi kata ya Matemanga wilayani humo.

Tukio hilo lilitokea Aprili 3 mwaka huu, kijiji cha Amani katika kata ya Nandembo wilayani humo ambapo marehemu huyo alikuwa akisafiria pikipiki aina ya Sunlg yenye namba za usajili T 886 CTC ambayo ilikuwa ikiendeshwa na mumewe huyo.

WAKULIMA TUNDURU WALALAMIKIA WATENDAJI WA VIJIJI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKULIMA katika kata ya Muhuwesi, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamewataka watendaji katika vijiji vya wilaya hiyo, kujenga ushirikiano wa karibu ili kuweza kusukuma mbele maendeleo yao. 

Rai hiyo ilitolewa na wakulima wa Chama cha ushirika cha Mumsasichema AMCOS, walipokuwa kwenye kikao chao cha wadau wa zao la korosho kilichofanyika katika ofisi za chama hicho kijiji cha Muhuwesi wilayani humo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Issa Kambutu alifafanua kuwa kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili ikiwemo kukithiri kwa vitendo vya wizi wa fedha za wakulima wa zao hilo, ukifanywa na baadhi ya viongozi hao sasa kuna kila sababu kujenga ushirikiano ili kuweza kudhibiti hali hiyo.

MUNDAU: FRELIMO ITAENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO WETU

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

IMEELEZWA kuwa ushirikiano uliopo kati ya wananchi wa vijiji vya Lunyere kilichopo wilayani Nyasa nchini Tanzania na Mpapa wilaya ya Lagunyasa jimbo la Lichinga Msumbiji, umetakiwa kudumishwa ili amani na utulivu uliopo mpakani kati ya nchi hizo mbili uweze kuendelea.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kumwapisha kamanda wa jumuiya hiyo kata ya Mpepo Bosco Kihwili, sherehe ambayo ilifanyika katika kijiji cha Lunyere.

Njowoka alisema wananchi wa Lunyere, hususani vijana wamekuwa wakijihusisha na shughuli za uchimbaji madini ambapo kutokana na uhusiano  mzuri uliopo kwa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili, wengi wao wamekuwa wakivuka mpaka na kwenda Msumbiji ambako pia hufanya shughuli za uchimbaji bila kikwazo hivyo ni vyema wakazingatia sheria zilizopo ambazo zinapaswa kufuatwa pindi wanapotaka kuingia nchi hiyo jirani.

Wednesday, April 15, 2015

KAMANDA WA VIJANA UVCCM NYASA ATOA MSAADA WA VITANDA KIJIJI CHA LUNYERE

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

KITENDO cha akina mama wajawazito kulala na kujifungulia chini ya sakafu katika Zahanati ya kijiji cha Lunyere, kata ya Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kimemshangaza Kamanda wa Jumuiya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia vifaa mbalimbali vinavyokosekana, hali ambayo itasaidia akina mama hao na wananchi kwa ujumla wapate huduma za afya katika mazingira salama.

Kushangazwa huko kulitokea baada ya kutembelea katika eneo hilo na kutoa msaada wa vitanda 20, magodoro 20, mito ya kulalia, mashuka na vyandarua vifaa ambavyo tokea ijengwe haikuwa navyo jambo ambalo lilisababisha wagonjwa wengi kupata huduma duni wanapokwenda kupata matibabu.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho wakati akikabidhi vifaa hivyo, Njowoka alisema ameguswa na kero hiyo inayowakumba wananchi hao ambapo analazimika kuendelea kutoa mingine ikiwemo mabomba ya maji, umeme wa nguvu ya jua na kukamilisha ukarabati wa chumba cha kujifungulia akina mama hao wajawazito.

WANAFUNZI WASOMEA CHINI YA MTI VIONGOZI NYASA WALAUMIWA

Watoto wakisoma chini ya mti.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

KAMANDA wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, Cassian Njowoka amesikitishwa na kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu wilayani humo kushindwa kutatua tatizo la ujenzi wa shule ya msingi Linda, ambayo imeezuliwa na upepo kitendo ambacho kinasababisha wanafunzi kukosa masomo darasani.

Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hivi sasa wanalazimika kusomea chini ya miti ya mikorosho, hali ambayo imekuwa ikiwapa kero kubwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nyakati hizi za masika.

Masikitiko hayo aliyatoa wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kuwasimika makamanda wa kata wilayani humo, ambapo alipofika katika kata ya Kilosa alielezwa tatizo la shule hiyo kuezuliwa na upepo Julai 11 mwaka jana.

Monday, April 13, 2015

WANAFUNZI NYASA HATARINI KUANGUKIWA NA JENGO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WATOTO wanaosoma katika shule ya msingi Nangombo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wapo hatarini kuangukiwa na majengo ya shule hiyo kutokana na kuwa chakavu na kutofanyiwa ukarabati kwa zaidi ya miaka 80.

Akizungumza na wazazi wa shule hiyo, Kamanda wa umoja wa vijana (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka alielezwa na mkuu wa shule hiyo, Hyasint Hyera kuwa majengo hayo ni machakavu na yapo hatarini kuanguka kufuatia kuwepo kwa nyufa sehemu mbalimbali.

Hyera alisema kuwa shule ilianzishwa mwaka 1932 na kwamba inawanafunzi 290 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, lakini pamoja na kutolewa taarifa mara kwa mara kwa viongozi wa serikali hakuna hatua zilizochukuliwa jambo ambalo ni hatari kwa watoto hao.

Alifafanua kuwa changamoto mojawapo inayowakabili shuleni hapo, ni kukosekana kwa vitendea kazi ikiwemo chaki za kuandikia pale mwalimu anapokuwa darasani akifundisha wanafunzi, hali ambayo ilisababisha watoto hao kukaa katika kipindi cha wiki tatu bila kufundishwa.

NYASA KUMUENZI KAPTENI KOMBA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

JUMUIYA ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, umeazimia kumuenzi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, Marehemu Kapteni John Komba kila mwaka ifikiapo Februari 28 wataandaa matamasha mbalimbali ikiwemo kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Aidha siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kuwakusanya, wananyasa waishio nje ya Nyasa, kurejea kwao na kusaidia kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo na maendeleo ya wananchi kwa ujumla ili waweze kuondokana na umasikini.

Kwa kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa maendeleo uliofanywa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kamanda wa jumuiya hiyo ya umoja wa vijana wilayani Nyasa, Cassian Njowoka alisema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo wakati alipokuwa akizungumza kwenye baraza la vijana kata ya Kilosa.

Thursday, April 9, 2015

KAYOMBO AIOMBA NMB KUONGEZA MASHINE ZA KUTOLEA FEDHA ILI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA WATU

Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo akizungumza katika semina ya siku moja ya Wadau wa kahawa ukumbi wa Jimbo katoliki Mbinga mjini, ambayo inaendeshwa na benki ya NMB, ambapo aliiomba benki hiyo katika kuboresha huduma zake iongeze kwa kujenga mashine za kutolea fedha (ATM) katika maeneo mbalimbali mjini humo, ili kupunguza msongamano wa watu katika benki hiyo. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga na kushoto ni Meneja wa Kanda ya kusini wa NMB, Lillian Mwinula.

WAKULIMA MBINGA WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI KATIKA ZAO LA KAHAWA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akifungua semina ya siku moja kwa Wadau wa kahawa wilayani humo kwenye ukumbi wa Jimbo katoliki uliopo mjini hapa, kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula na upande wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo.

Baadhi ya Wadau wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakifuatilia mada kwa umakini katika semina ya wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika leo ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuongeza uzalishaji katika zao hilo, ili waweze kujiongezea kipato na hatimaye waweze kuondokana na umasikini.

Aidha wameaswa kuzingatia kununi bora za kilimo kwa kushirikiana na wataalamu wa zao hilo, ili wafikie lengo la uzalishaji wa kahawa bora na yenye kupata soko na bei nzuri mnadani.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alitoa rai hiyo leo katika semina ya siku moja ya Wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa ambayo ilikuwa ikiendeshwa na benki ya NMB tawi la Mbinga.

Ngaga alisema kuwa wakulima wa zao hilo, wanakila sababu ya kuelimishwa juu ya kilimo bora cha kahawa ili waweze kuzalisha zaidi, na kuifanya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla liweze kusonga mbele kimaendeleo.

BENKI YA NMB YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA KAHAWA MBINGA

Upande wa kushoto, Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akikaribishwa leo katika ukumbi wa Jimbo Katoliki uliopo mjini hapa na Meneja wa benki ya NMB tawi la Mbinga Lugano Mwampeta, kwa ajili ya kufanya ufunguzi wa semina ya siku moja kwa wadau wa kahawa wa wilaya hiyo. Anayeshuhudia tukio hilo ni Meneja wa benki hiyo tawi la Litembo wilayani Mbinga, Victor Msoffe.

Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula, akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma, Gaudence Kayombo ambaye alikuja kushiriki katika semina ya Wadau wa kahawa inayofanyika leo kwenye ukumbi wa Jimbo Katoliki mjini hapa. Kwa ujumla semina hiyo inaendeshwa na benki hiyo kwa manufaa ya kumuinua mkulima kiuchumi ili aweze kuondokana na umasikini. 

Wednesday, April 8, 2015

KUMBURU AZITAKA HALMASHAURI KUTUNGA SHERIA NDOGO ZA UENDESHAJI CPU

 
Adolph Kumburu, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake na Wadau wa zao hilo, hapa nchini.
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKURUGENZI wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Adolph Kumburu, amesema kuwa msimu wa mavuno ya zao hilo hapa nchini umefunguliwa mapema mwezi Aprili mwaka huu, kutokana na baadhi ya maeneo ambayo yanawahi kuiva zao hilo wakulima waweze kuuza kahawa yao mapema bila kuchelewa.

Aidha msimu huu wa mwaka 2015/2016 bodi imefanya makadirio ya kukusanya tani 60,000 tofauti na msimu wa mwaka 2014/2015 ilikadiria kukusanya tani 44,000 lakini haikufikia lengo hilo, badala yake ilikusanya tani 43,000 tu jambo ambalo alifafanua kuwa lilitokana na baadhi ya maeneo hapa nchini zao hilo kushambuliwa na wadudu waharibifu, na kusababisha kushindwa kufikia malengo husika.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi huyo, alipokuwa kwenye mkutano wa Wadau wa zao la kahawa mkoani Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo wilayani Mbinga mkoani humo.

MTOTO APOTEZA MAISHA BAADA YA KUTAFUNWA NA WANYAMA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MTOTO wa mfugaji mwenye asili ya Kisukuma, walioweka makazi katika kijiji cha Twendembele kata ya Ligunga wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, aliyefahamika kwa jina la Shija Luchoma (15) amefariki dunia na mwili wake kuliwa na wanyama wakali, baada ya kuvamiwa wakati akichunga ng’ombe porini katika kijiji hicho.

Taarifa za tukio hilo, zinafafanua kuwa marehemu huyo alikumbwa na mkasa huo baada ya kushambuliwa na mnyama ambaye bado hajafahamika, wakati akiwa machungani kwenye hifadhi ya Selou kijijini humo.   

Baba mzazi wa kijana huyo, Masanja Luchoma alisema tukio lilitokea Machi 26 mwaka huu ambapo marehemu alikuwa ameondoka nyumbani kwake na kundi la ng’ombe hao kwa ajili ya kwenda kuwachunga waweze kupata malisho, ambapo baadaye ilimshangaza mnamo majira ya jioni aliona ng’ombe wakiwa wanarudi peke yao.