Saturday, April 18, 2015

WAFARIKI DUNIA NA WENGINE 20 KUJERUHIWA VIBAYA KATIKA AJALI YA GARI WAKIELEKEA MNADANI

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 20 kujeruhiwa vibaya, kufuatia ajali ya gari aina ya Mitsubishi Fuso kupinduka katika kijiji cha Burma wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo kumshinda kona za milima ya Ambrose zilizopo katika kijiji hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema kuwa ajali hiyo, imetokea leo majira ya saa 3:30 asubuhi katika kijiji hicho wilayani humo.

Msikhela alifafanua kuwa gari hilo lilikuwa likitokea Songea kwenda Mbamba bay, wilaya ya Nyasa huku likiwa limebeba watu hao, pamoja na mizigo kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli za mnada.

Kadhalika alieleza kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Erick Owiso, ambapo majeruhi 18 wamelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga na wawili ambao ni Ignas Ndonde na Meshack Mlinya, wamepelekwa katika Hospitali ya Peramiho iliyopo wilaya ya Songea kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Vilevile aliwataja waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo kuwa ni, Samwel Ngonyani (25) na Rainel Ndonde (28) wote wakazi wa Songea mjini na maiti hizo zimehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga, zikisubiri kusafirishwa kwenda makwao.

Pamoja na mambo mengine Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Msikhela ametoa wito kwa wamiliki wa magari ya mizigo mkoani humo kuacha tabia ya kubeba mizigo na abiria ndani ya magari hayo, jambo ambalo alieleza kuwa linahatarisha usalama wao na kusababisha ajali au vifo visivyokuwa vya lazima.

No comments: