Wednesday, April 1, 2015

GAUDENCE KAYOMBO ARUSHIWA KOMBORA NA WAPIGA KURA WAKE, WAMTAKA AFUTE KAULI KWAMBA HAKUNA MKULIMA ANAYELALAMIKA JUU YA WIZI WA KAHAWA

Gaudence Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki ambaye analalamikiwa na wapiga kura wake kwamba anatetea hakuna wizi wa kahawa uliofanyika kwa wakulima wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, jambo ambalo wanamshangaa na kumtaka afute kauli yake huku wakiiomba serikali iingilie kati ili waliohusika na hujuma hiyo wachukuliwe hatua za kisheria. 
Na Kassian Nyandindi,

WAKULIMA wanaozalisha zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wamesema wanamshangaa Mbunge wao wa Jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo kwamba hakuna mkulima anayelalamika juu ya wizi wa fedha baada ya kahawa yao kuuzwa mnadani Moshi, hivyo wamemtaka afute kauli hiyo na kushughulikia matatizo ya wananchi wa jimbo hilo, na sio kukaa kupinga malalamiko yanayotolewa na wananchi wake huku akijua fika kufanya hivyo ni kuendelea kuitesa jamii.

Kwa nyakati tofauti walisema wamekosa imani naye baada ya Mbunge huyo hivi karibuni kusikika kwenye vyombo vya habari, TV na Magazeti akikanusha na kusema wakulima hao wamenufaika na mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na hakuna aliyeibiwa fedha, ambapo ni muda mrefu sasa umepita pamoja na kufikishiwa malalamiko hayo mezani kwake juu ya wizi waliofanyiwa wakulima hao lakini hakuna hatua aliyochukua huku wakiongeza kuwa, huenda anamaslahi yake binafsi ndio maana amekuwa akitumia muda mwingi kutetea jambo hilo.

Walifafanua kuwa umefika wakati sasa, kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kuacha tabia ya kutetea watendaji wa serikali ambao ni wezi wakiwaibia wakulima wanyonge na endapo ataendelea kufanya hivyo, ni sawa na kuwatesa wapiga kura wake na kuwanyima fursa za kimaendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

“Huyu Mbunge sisi tunamshangaa sana, anafikia hatua anadanganya watu kupitia vyombo vya habari kwamba hakuna mkulima anayelalamika katika jimbo lake ameibiwa fedha baada ya kahawa kuuzwa mnadani yeye anawezaje kuthibitisha hili, hivyo asubiri mwarobaini wake ataupata uchaguzi mkuu ujao”, walisema.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa, Mbunge Kayombo amefikia hatua ya kutoa kauli hizo baada ya Mkurugenzi wake, Hussein Ngaga na viongozi wa vyama vya ushirika, kulalamikiwa na wakulima wa kahawa wilayani Mbinga kupitia vyombo vya habari kuwa wanadaiwa kuwaibia shilingi milioni 783,399,412 katika sehemu ya kahawa zao ambazo waliuza huko mnadani Moshi.

Wakulima hao ni wale ambao walikopeshwa fedha shilingi bilioni 2 na shirika hilo la NSSF kupitia vyama vyao vya ushirika (AMCOS) vilivyopo wilyani humo, ambapo lengo la shirika lilikuwa ni kutoa mikopo yenye gharama nafuu kwa wakulima wadogo wadogo ambao wamejiunga kisheria katika vikundi, hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na waondokane na umasikini.

Malalamiko haya yanafuatia pia, Mkurugenzi huyo kuingilia kati na kupangia matumizi ya fedha juu ya mkopo huo ambao wakulima walikopeshwa, jambo ambalo mpaka sasa amekuwa hataki kutoa hata mwenendo wa fomu ya mauzo ya kahawa zao (Account Sale) ili wakulima waweze kujua hatma ya kahawa yao jinsi gani ilivyouzwa huko mnadani.

“Tumekuwa tukinyimwa hata mwenendo wa matumizi ya fedha zetu tulizokopeshwa na NSSF ambazo ziliingizwa katika akaunti zetu za vyama vya ushirika (Bank Statement) ili tuweze kujua zimetumikaje, kwa sababu wakati wa manunuzi ya kahawa mkurugenzi huyu alikuwa akitupangia matumizi tunakwenda kuchukua fedha benki mpaka ruhusa itoke kwake na kiasi anachotaka yeye, sasa tunahoji hivi kweli hizi ndizo taratibu na sheria za vyama vya ushirika zinavyosema?”, walihoji.

Pamoja na mambo mengine, wakulima wanaolalamikia juu ya hali hiyo wanatoka katika vyama vinne vya ushirika ambavyo ni Mahilo, Ngaka, Ngima na Pilikano ambapo hata viongozi wao wa ushirika nao wanalalamikiwa kwamba wameshirikiana na Mkurugenzi Ngaga kwa namna moja au nyingine kuhujumu fedha hizo za wakulima wa kahawa, huku wakiiomba serikali kuingilia kati ili haki zao ziweze kupatikana.

KAYOMBO ARUSHIWA KOMBORA

Wakulima hao ambao walionekana kuendelea kujawa na jazba, waliibua jipya huku wakiendelea kumrushia kombora Mbunge wao Kayombo wakisema kuwa, mnamo mwezi Agosti mwaka 2012 alianzisha umoja wa wakulima wa kahawa unaofahamika kwa jina maarufu la; Mbinga Umoja Coffee Association, ambao ulilenga wakulima wa kahawa wilayani humo waweze kufanya biashara ya kuuza kahawa yao kwa bei nzuri nchi za nje.


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, vikundi ambavyo vilisajiliwa na idara ya maendeleo ya jamii wilayani hapa, vilichangishwa fedha nyingi na kuingizwa ndani ya umoja huo lakini hakuna maendeleo yaliyozaa matunda.

Mbunge huyo anashutumiwa kwamba, alikuwa akitumia hata fedha za mfuko wa jimbo kuendeshea umoja huo huku akitambua anakiuka taratibu na ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi, ambazo ilibidi zikafanye shughuli husika.

Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na Mwenyekiti wa umoja huo, Aidan Turuka alithibitisha juu ya Kayombo kuwapatia fedha shilingi milioni 7,700,000 kutoka katika mfuko huo wa jimbo, ambazo hutolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi.

Jitihada zilizofanywa na mwandishi wetu, zilifanikiwa kupata bank statement yenye kuonyesha siku fedha hizo zilipoingizwa kwenye akaunti ya umoja huo, namba 61710000760 benki ya NMB tawi la Mbinga.

Tarehe 22 mwezi Juni, mwaka 2012 fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo kupitia mfumo wa hundi na baadaye kutolewa kidogo kidogo, kwa ajili ya matumizi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya umoja. 

Walifafanua kuwa baada ya umoja huo, kukusanya kahawa nyingi za wakulima ambazo zilikobolewa kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga (MCCCO) na kuhifadhiwa katika ghala la Makambako mkoani Njombe kwa muda mrefu, huku Mbunge huyo akiwadanganya wakulima kuwa anatafuta masoko nje ya nchi ili ikauzwe kwa bei nzuri na kuwazuia wasipeleke mnadani Moshi.

Lakini mwishoni alikosa soko na kusababisha hasara kwa wakulima, na kulazimika kahawa kuuzwa huko mnadani kwa bei ya chini kutokana na kukaa muda mrefu bila kuuzwa huku mnada wa mauzo ukiwa umepita, jambo ambalo lilisababisha wakulima wengi wilayani Mbinga, kupata hasara na kudaiwa na benki ya NMB ambako walikopa fedha kwa ajili ya kuendeshea biashara hiyo ya kahawa.

Baadhi ya wakulima wamepata hasara kufuatia mali zao ambazo waliwekea dhamana benki, kupigwa mnada na kuuza kwa bei ya hasara ili kufidia deni walilokuwa wakidaiwa na benki hiyo.

Pia kufuatia hali hiyo imefanya umoja huo ufe kifo cha mende na Kayombo kubuni mbinu mpya kukimbilia Shirika la NSSF kushawishi, ili wakulima wakopeshwe fedha kwa ajili ya kununulia kahawa na leo wanaibiwa tena ndio maana kumekuwa na mwendelezo wa malalamiko ya hapa na pale.

Kutokana na mambo hayo wakulima wengi wa kahawa wilayani humo, wamesema wamechoshwa na kauli za Mbunge huyo kutetea masuala ambayo hayana tija kwao, hivyo wameapa kamwe hawataweza kuendelea kuvumilia mateso wanayopata sasa na yeye akiendelea kutetea watu wanaowaibia wakulima wanyonge, ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi jembe la mkono kuzalisha mazao shambani ili maisha yao yaweze kusonga mbele.


Hivi karibuni alipotafutwa Kayombo ili aweze kuzungumzia juu ya madai haya alisema kuwa, anashangaa kwa nini malalamiko hayo yanatokea kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu hivyo haoni haja ya wao kumuadhibu.

No comments: