Friday, April 17, 2015

KAMANDA UVCCM AISAMBARATISHA CHADEMA NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Mbamba bay.

BAADHI ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamekiasi chama hicho na kuhamia Chama Cha Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichoeleza kuwa, wamechoshwa na sera za Chadema ambazo zimekuwa zikichochea machafuko mara kwa mara hapa nchini.

Wafuasi hao ambao walikuwa 67 walieleza kuwa, hawana sababu ya kuendelea kuwa katika chama hicho cha upinzani badala yake waliona ni heri warejee kwenye chama mama, CCM ambako walikuwa tokea awali.

Hali hiyo ilitokea leo katika viwanja vya mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo, kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na Kamanda wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa, Cassian Njowoka.


Aidha katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa mji huo, kelele na shangwe za hapa na pale zilirindima katika viwanja hivyo huku wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi, wakiwapokea wenzao wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwa furaha wakati wanarudisha kadi zao za chama hicho cha upinzani.

Akizungumza na wananchi waliokusanyika kusikiliza mkutano huo, ambao ulilenga kumsimika rasmi kamanda wa UVCCM wa kata ya Mbamba bay, Kamanda wa Jumuiya hiyo wilaya ya Nyasa Njowoka alisema kuwa, jambo muhimu kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni kujenga ushirikiano imara katika kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

“Ndugu zangu nawasisitiza, tunapaswa wote kwa pamoja kujenga wilaya yetu kwa faida ya baadaye, hatupaswi kubaguana au kujenga matabaka yasiyokuwa na lazima katika jamii”, alisema.

Pia Njowoka alitoa ahadi ya vitanda 20, magodoro 20 na mashuka yake ya kujifunika wagonjwa katika Hospitali ya wilaya ya Nyasa, ambayo inakabiliwa na upungufu wa vifaa hivyo.


Vilevile katika Hospitali hiyo, alisema atawapatia kitanda kimoja cha kujifungulia akina mama wajawazito ili kiweze kuwasaidia akina mama hao, wakati wa kujifungua.

No comments: