Thursday, April 9, 2015

WAKULIMA MBINGA WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI KATIKA ZAO LA KAHAWA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akifungua semina ya siku moja kwa Wadau wa kahawa wilayani humo kwenye ukumbi wa Jimbo katoliki uliopo mjini hapa, kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya kusini Lillian Mwinula na upande wa kulia ni Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo.

Baadhi ya Wadau wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakifuatilia mada kwa umakini katika semina ya wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika leo ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuongeza uzalishaji katika zao hilo, ili waweze kujiongezea kipato na hatimaye waweze kuondokana na umasikini.

Aidha wameaswa kuzingatia kununi bora za kilimo kwa kushirikiana na wataalamu wa zao hilo, ili wafikie lengo la uzalishaji wa kahawa bora na yenye kupata soko na bei nzuri mnadani.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alitoa rai hiyo leo katika semina ya siku moja ya Wadau wa kahawa wa wilaya hiyo, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jimbo katoliki mjini hapa ambayo ilikuwa ikiendeshwa na benki ya NMB tawi la Mbinga.

Ngaga alisema kuwa wakulima wa zao hilo, wanakila sababu ya kuelimishwa juu ya kilimo bora cha kahawa ili waweze kuzalisha zaidi, na kuifanya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla liweze kusonga mbele kimaendeleo.


“Tuelimishe wakulima wetu, waache kilimo cha mazoea tukiwa na dhana hii ya kilimo cha biashara katika zao hili, ndugu zangu nina hakika tutafika katika malengo yetu na kusonga mbele zaidi”, alisema Ngaga.

Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya wilaya ya Mbinga hutokana na kilimo cha zao hilo, hivyo wadau wa kahawa amewasisitiza kuendelea kuliboresha kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Awali akizungumza katika semina hiyo Meneja wa Kanda ya kusini benki ya NMB, Lillian Mwinula alisema kuwa lengo kuu la benki hiyo ni kuona kilimo cha zao hilo kinamwinua mkulima, ili aweze kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo hukabiliana nazo katika maisha yake ya kila siku.


Mwinula alisema benki hiyo inafanya kazi zake kwa uwazi na kauli mbiu yake; Kilimo ni biashara, ikiwa ni lengo la kuhamasisha wakulima waweze kuzalisha mazao kwa wingi na ubora zaidi.

No comments: