Wednesday, April 15, 2015

WANAFUNZI WASOMEA CHINI YA MTI VIONGOZI NYASA WALAUMIWA

Watoto wakisoma chini ya mti.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

KAMANDA wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, Cassian Njowoka amesikitishwa na kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu wilayani humo kushindwa kutatua tatizo la ujenzi wa shule ya msingi Linda, ambayo imeezuliwa na upepo kitendo ambacho kinasababisha wanafunzi kukosa masomo darasani.

Wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo hivi sasa wanalazimika kusomea chini ya miti ya mikorosho, hali ambayo imekuwa ikiwapa kero kubwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nyakati hizi za masika.

Masikitiko hayo aliyatoa wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kuwasimika makamanda wa kata wilayani humo, ambapo alipofika katika kata ya Kilosa alielezwa tatizo la shule hiyo kuezuliwa na upepo Julai 11 mwaka jana.

Njowoka alisema ni jambo la kushangaza kuona shule hiyo imekaa kwa muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati, jambo ambalo alifafanua kuwa ni uzembe uliokithiri ambao haupaswi kuvumiliwa hivyo aliwaasa viongozi wa wilaya ya Nyasa, kujenga tabia ya kutembelea shule za msingi na sekondari ili kubaini changamoto mbalimbali na kuzipatia utatuzi kwa wakati.

Alisema yeye akiwa Kamanda wa vijana, tatizo hilo limemgusa kwani UVCCM kamwe haiwezi kuona chipukizi wake ambao baadaye watakuwa wanachama wake wanapata shida, hivyo aliamua kuchangia bati 90 ili zisaidie kuezekea shule hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Linda wilayani Nyasa, Essau Ndunguru alieleza kuwa jengo hilo lililoezuliwa ni la vyumba vitatu, ambalo lilikuwa likitumika kusomea watoto wa darasa la nne, tano na la saba ambapo takribani wanafunzi 140 wanakosa sehemu ya kusomea kutokana na kukumbwa na maafa hayo.

Ndunguru alifafanua kuwa, kutokana na kukosa fedha kwa muda mrefu za kuendelea na ujenzi huo ndio kumesababisha kukwama, na hivyo watoto hao kuendelea kukumbwa na adha hiyo.

“Watoto hivi sasa wanasomea chini ya miti ya mikorosho, ambayo ipo hapa jirani na shule yetu kutokana na jengo hili walilokuwa wakilitumia kusomea kuezuliwa na upepo mkali, tunaiomba serikali na wadau mbalimbali waone namna ya kutusaidia juu ya kumaliza tatizo hili ili tuweze kuondokana na usumbufu tunaoupata sasa”, alisema Ndunguru.


Hata hivyo mwalimu huyo aliwaasa wazazi na walezi wa kijiji cha Linda kujitokeza bila kusukumwa kuchangia nguvu zao, pale wanapotakiwa ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu jambo litakalowafanya waweze kuishi jirani na mazingira ya shule tofauti na ilivyo sasa, hulazimika kuishi uraiani.

No comments: