Monday, April 6, 2015

RUSHWA YA FEDHA NA MIKAKATI YA UPOTOSHWAJI UFUFUO WA YESU

Padre Baptiste Mapunda.
 Na Padre Baptiste Mapunda,

PASAKA ni sikukuu ya kusherehekea “ushindi wa Yesu” dhidi ya mauti, dhidi ya maovu ya kila aina yanayomshambulia mwanadamu kwa wale wanaomwamini. Yesu amefufuka kweli, kweli kama alivyosema, hayupo kaburini yu hai.

Ujumbe huu ni mzito na wa kushitua ulimwengu wote, hasa kwa waliowakristo na wasiowakristo.

Jumapili ya Pasaka nilisherehekea Parokiani Manzese na ibada ilikuwa na mahudhurio makubwa, pamoja na hamasa ya hali ya juu. Ibada siku zote zinatujenga sana kama mashahidi wa ufufuko wa Kristo.

Jumatatu ya Pasaka nilikuwa na ratiba ya kuhudhuria misa ya saa tatu, ambayo ilikuwa ni ya ubatizo na ndoa. Lakini nikajikuta nasukumwa kwenda kuhudhuria misa ya saa moja, ambayo ilikuwa ni ya wanaumini wa kawaida. Nilipofika Kanisani nilimkuta Padre na mwanashirika mwenzangu, Padre Alex Mutasingwa  ambaye alikuwa kiongozi ibada. 


Kilipofika kipindi cha mahubiri, Padre Alex alinichoma sana pale alipozungumzia juu ya matumizi ya rushwa ya fedha waliyohongwa maaskari, waliokuwa wakilinda kaburi la Yesu, ili wadanganye kwamba “walipokuwa wamelala basi wafuasi wake walikuja  kumwiba.”

Ufufuko wa Yesu ulikuwa ni tishio na mwiba kwa uongozi wa Kiyahudi, kwani wao hawakusadiki kama kweli Yesu alikuwa ni mwana wa Mungu, ambaye angefufuka siku ya tatu.

Wakuu wa Mayahudi baada ya kupata habari kwamba Yesu hayumo kaburini, walifadhaika sana na hivyo kutafuta haraka sana, njia ya kupotosha ukweli wa ufufuko huo ambao ulikuwa n ushindi dhidi ya fitina yao ya kumuua.

Mbinu chafu waliyopanga ni pale viongozi hao wa Mayahudi, kuwaambia  maaskari polisi kwamba “ninyi chukueni pesa hii na mseme kwamba  tulipokuwa tumelala wafuasi wake walikuja kumwiba usiku.” Na viongozi hao waliapa kuwalinda maaskari hao ili wasisumbuliwe na jamii.

Hadi leo hii dunia na jamii yetu, askari polisi wanaendelea kutumiwa ili kupotosha  ukweli kwa rushwa ya pesa. Je, hii inatokana na laana ya pesa iliyomtoa Yesu mwenyewe?                                                

UKWELI DAIMA UTASHINDA kwani Yesu hatimaye alijitokeza kwa wafuasi wake na salamu ya amani kwenu msiogope, akajidhihirisha kwamba hajaibiwa bali amefufuka katika wafu. Yesu anatibu sumu ya rushwa kwa kutumia ukweli kwamba yeye amefufuka. Habari hii ni mbaya kwa maadui.

Maandiko matakatifu huwalaani na kuwakaripia Mahakimu na Polisi ambao wanadhamana kubwa ya kusimamia, HAKI NA UKWELI BILA KUPENDELEA. Hii inatokana na ukweli kwamba Mungu wa Wana wa Waisraeli, hapendelei nyuso za watu (kumb 10:17). Mwalimu Nyerere alisema Rushwa ni adui wa haki.

Inaonekana wazi kwamba rushwa ya maaskari, ilianza sikukuu ya ufufuko wa Bwana. Na hii yote walifanya ili kupotosha ukweli kwamba, Yesu amefufuka tukio ambalo lilikuwa ni aibu kwa viongozi wa Kiyahudi, lakini kwa waliomwamini ulikuwa ni ushindi wa kishindo.

Mungu bado anaendelea  kuichukia rushwa, anapowakaripia viongozi na wenye madaraka kwamba “wewe usipokee rushwa, huwapofusha hao waonao na kuyapotosha maneno ya wenye haki” (Kumb 23:18). Pasaka hutufundisha kwamba rushwa inauwezo wa kupotosha ukweli hata hivyo ilishindikana kabisa.

Je, katika nchi yetu propganda za kisiasa ni sehemu ya kuupotosha ukweli? Kiongozi anayepokea rushwa hukosa heshima, na baraka ya kuwatumikia watu waliompa dhamana.

Viongozi wa ngazi zote katika jamii yetu yaani serikali, vyama vya siasa, taasisi na madhehebu ya dini ni jukumu letu kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa haki, hasa haki kwa maskini. Nabii Isaya  anaonya kwa kusema bayana kwamba “viongozi wa Israeli hawajali chochote kwa dhiki za wanyonge, huwanyang’anya haki zao.” Je hapa nchini hali ipoje?

Wajibu wa Manabii kuwaonya viongozi wa jamii, juu ya haki ya wanyonge inayoathiriwa na rushwa.

Nikirudi katika tafakari ya Padre Alex Mutasingwa, Jumatatu ya Pasaka kanisani Manzese ilinichoma sana wakati aliposisitiza juu ya ujasiri wa viongozi kusimamia ukweli. Siku hizi katika jamii yetu baadhi ya viongozi wapo tayari kupokea  rushwa na kutoa viapo kwa Mungu na jamii kwa ujumla, ili kuuangamiza ukweli na haki  kama walivyofanya siku ya  ufufuko wa Yesu Kristo.

Ni mara ngapi watu wanasimama kusema uwongo hata Mahakamani, ili kupotosha na kupindisha ukweli? Leo ukiichunguza nchi yetu unakuta mivurugano ya kila aina, na wananchi wamejaa malalamiko na huzuni za kila aina.

Maovu na machafuko yametawala kila kukicha. Matumizi ya rushwa yanaonekana kuliangamiza taifa letu, bila watawala kujua cha kufanya. Swali langu ni hili  kwa nini  viongozi wahusika  wanaogopa kuusimamia ukweli?

Mtume Petro mara baada ya kwenda kaburini na kubaini kwamba Yesu kweli alikuwa amefufuka, aliamini. Kuamini huku kulimpatia nguvu  ya kwenda kwa wale maadui wa Yesu waliomuua na kueneza uwongo kwamba alikuwa ameiibiwa.

Petro anapata ujasiri wa kuwaambia ukweli kwamba, “yule aliyefufuka  msipoteze muda wa kutafuta tafuta ni nani, kwani ni yule yule, mliyemdharau, mliyemkejeli, mliyemtukana na kumdhihaki na mliyemwambia msalabani, ni Yesu kristo  aliyefufuliwa na nguvu ya Mungu.

Katika hili Petro naye alikuwa amejipatia ujasiri wa kuufika ukweli, kwa sababu “ukweli unakuweka huru” (Rumi 8:31).
Tunapoendelea kushereka sikukuu hii ya Pasaka, ambayo ni sikukuu ya ushindi wa Yesu dhidi ya uwongo na maovu basi  nasi tubadilishwe na nguvu ya ufufuko wa Yesu Kristo.

Nchi yetu inayopita katika kipindi hiki kigumu hasa katika nyanja ya kiuchumi, kijamii, kiutumaduni, kiimani na kisiasa juu ya suala la katiba mpya na mitifuano iliyopo ya mahakama ya kazi, tunahitaji iongozwe na ukweli.

Namaliza kwa kusema “nchi yetu itakombolewa na viongozi wenye ujasiri wa kusimamia ukweli toka mwanzo hadi mwisho, bila kuyumbishwa na pesa wala vyeo kama walivyoonyesha Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo, katika suala la upigaji kura ya hapana kwa katiba pendekezwa.

Halikadhalika Yesu na Petro wanatufundisha kwamba rushwa ni kansa ya roho na akili, ni lazima tutumie nguvu ya Mungu katika kuitibu.
Nawatakieni Pasaka njema yenye amani, furaha, upendo, matumaini na maisha  mapya.


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; Frmapunda91@gmail.com

No comments: