Wednesday, April 8, 2015

APOTEZA MAISHA BAADA YA KUSHAMBULIWA NA VIBAKA

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

SAID Chalres ambaye ni mzee mwenye umri wa miaka 58, mkazi wa kitongoji cha Nanjati kata ya Muhuwesi wilaya ya Tunduru mkoani hapa, ameshambuliwa na baadhi ya vijana ambao wanadaiwa kuwa ni vibaka na kumsababishia afariki dunia.

Vibaka hao walimshambulia mzee huyo, kwa kumpiga mangumi na mateke, kwa lengo la kumpora shilingi 10,000, radio, simu na dagaa ambao alikuwa anatoka kuwanunua katika gene lililopo karibu na kitongoji hicho.

Mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa, wakati anarudi akiwa njiani ndipo walimvamia na kumnyang’anya vitu hivyo na fedha hizo ambazo alikuwa nazo mfukoni.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Diwani wa kata hiyo Nurdin Mnolela mbali na kuthibitisha juu ya tukio hilo aliongeza kuwa watuhumiwa baada ya kutimiza adhma yao, walitokomea kusikojulikana.


Vilevile alifafanua kuwa baada ya yeye kupata taarifa hizo, alipiga simu kituo cha Polisi wilaya ya Tunduru kwa msaada zaidi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa watuhumiwa wanasakwa ili waweze kupatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pamoja na mambo mengine, Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Charles, Dokta Titus Tumbu alisema kifo cha mzee huyo kilisababishwa na kipigo kikali na kutokwa na damu nyingi.

Katika tukio jingine, Polisi wanamtafuta dereva wa gari aina ya Isuzu, kwa kosa la kusababisha mauaji ya mtembea kwa miguu aliyefahamika kwa jina la John Katiasi (40) ambaye alimgonga na lori hilo la mizigo.

Kamanda huyo wa polisi mkoani hapa, alisema dereva huyo ambaye jina lake bado halijahamika baada ya kusababisha mauaji hayo, aliutelekeza mwili wa marehemu huyo na kukimbia na gari hilo.


Tukio lilitokea Marchi 27 mwaka huu, majira ya usiku katika kijiji cha Namakambae katika tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru.

No comments: