Wednesday, April 15, 2015

KAMANDA WA VIJANA UVCCM NYASA ATOA MSAADA WA VITANDA KIJIJI CHA LUNYERE

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

KITENDO cha akina mama wajawazito kulala na kujifungulia chini ya sakafu katika Zahanati ya kijiji cha Lunyere, kata ya Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kimemshangaza Kamanda wa Jumuiya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia vifaa mbalimbali vinavyokosekana, hali ambayo itasaidia akina mama hao na wananchi kwa ujumla wapate huduma za afya katika mazingira salama.

Kushangazwa huko kulitokea baada ya kutembelea katika eneo hilo na kutoa msaada wa vitanda 20, magodoro 20, mito ya kulalia, mashuka na vyandarua vifaa ambavyo tokea ijengwe haikuwa navyo jambo ambalo lilisababisha wagonjwa wengi kupata huduma duni wanapokwenda kupata matibabu.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho wakati akikabidhi vifaa hivyo, Njowoka alisema ameguswa na kero hiyo inayowakumba wananchi hao ambapo analazimika kuendelea kutoa mingine ikiwemo mabomba ya maji, umeme wa nguvu ya jua na kukamilisha ukarabati wa chumba cha kujifungulia akina mama hao wajawazito.


Njowoka aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Lunyere, kwa kuchangishana shilingi milioni 40 ambazo zimetumika kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo huku akiutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, kuunga mkono juhudi zilizofanywa na wananchi wa kijiji hicho ambacho kipo upande wa kusini mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

“Ningependa kuona kambi ya vijana wa kata hii ya Mpepo wanaiweka hapa Lunyere, lakini kazi kubwa iwe kujishughulisha jambo ambalo litakuwa msaada katika kukamilisha ujenzi wa zahanati hii, ikiwemo kufyatua tofari zitakazosaidia ujenzi wa nyumba za kuishi waganga”, alisema Njowoka.

Awali kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Anderson Haulle alisema mpaka kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo hakuna mchango wowote uliotolewa na serikali, jambo ambalo linawasikitisha wananchi na kujiona kama wametengwa na viongozi wao waliowachagua na watendaji wa Halmashauri hiyo,  ambao wamepewa dhamana ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Haulle alisema Lunyere ni kijiji ambacho wanaishi wachimbaji wa madini ambapo moja ya kero waliyokuwa wakikabiliana nayo kabla ujenzi wa zahanati hiyo, ni kutokea kwa vifo vingi na maiti zilikuwa zinahifadhiwa katika ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho kitendo ambacho kimsingi ni udhalilishaji wa binadamu.

Naye Mganga mkuu wa zahanati hiyo, William Ndimbo alifafanua kuwa magonjwa yaliyoshamiri kijijini hapo ni malaria, kuharisha, kichomi, magonjwa ya zinaa na Ukimwi na kwamba changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa madawa ambapo kutokana na kituo kutosajiliwa na Bohari ya madawa ya binadamu (MSD) hulazimika kupata madawa kutoka wilayani.


Hata hivyo Ndimbo alimshukuru Kamanda huyo wa Jumuiya ya umoja wa vijana kutokana na moyo wake wa kutoa vifaa hivyo, na kwamba ahadi yake ya kutoa madawa yenye thamani ya shilingi milioni moja kila mwaka itasaidia kutoa kero ya upatikanaji wa madawa, huku akiwataka wadau wengine nao wajitokeze kusaidia ili waweze kuondokana na matatizo mbalimbali wanayokabiliana nayo katika sekta hiyo ya afya.

No comments: