Thursday, April 30, 2015

DEREVA WA PIKIPIKI MBINGA APANDISHWA KIZIMBANI KWA KULAWITI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

LAURENT Kibasa (30) ambaye ni dereva wa pikipiki, mkazi wa mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya hiyo, kwa tuhuma ya kumlawiti mwanaume mwenzake (Jina tunalo) mwenye umri wa miaka 24 na kumdhuru mwili.

Mwendesha mashtaka msaidizi wa polisi, Inspekta Seif Kilugwe alidai mbele ya Hakimu Joachimu Mwakyolo wa Mahakama ya wilaya ya Mbinga, kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 23 mwaka huu majira ya mchana akiwa nyumbani kwake baada kushindwa kulipwa deni analodai shilingi 85,000.

Kibasa anadaiwa kufanya makosa hayo kwa dereva wa pikipiki mwenzake maarufu kwa jina la Boda boda, baada ya kumfuata kwenye eneo lake la kazi kisha kumkamata na kumpeleka nyumbani kwake ambako anadaiwa alimfunga kamba mikononi na kuanza kumpiga, kwa kutumia mkanda wake wa suruali.


Inspekta Seif alieleza Mahakamani hapo kuwa, mshtakiwa huyo wakati anafanya hilo pia alikuwa akimpiga kwa mateke na ngumi na baadaye alimbeba na kumpeleka chooni, ambako alimvua suruali aliyokuwa ameivaa na kumfanyia kitendo hicho cha kinyama.

Pamoja na mambo mengine, Kibasa amekwisha somewa maelezo hayo ya awali na alikana shitaka hilo linalomkabili na kwamba limepangwa kusikilizwa tena, Mei 5 mwaka huu na mshatakiwa yupo nje kwa dhamana.

No comments: