Monday, April 13, 2015

WANAFUNZI NYASA HATARINI KUANGUKIWA NA JENGO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

WATOTO wanaosoma katika shule ya msingi Nangombo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wapo hatarini kuangukiwa na majengo ya shule hiyo kutokana na kuwa chakavu na kutofanyiwa ukarabati kwa zaidi ya miaka 80.

Akizungumza na wazazi wa shule hiyo, Kamanda wa umoja wa vijana (UVCCM) wa wilaya hiyo, Cassian Njowoka alielezwa na mkuu wa shule hiyo, Hyasint Hyera kuwa majengo hayo ni machakavu na yapo hatarini kuanguka kufuatia kuwepo kwa nyufa sehemu mbalimbali.

Hyera alisema kuwa shule ilianzishwa mwaka 1932 na kwamba inawanafunzi 290 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, lakini pamoja na kutolewa taarifa mara kwa mara kwa viongozi wa serikali hakuna hatua zilizochukuliwa jambo ambalo ni hatari kwa watoto hao.

Alifafanua kuwa changamoto mojawapo inayowakabili shuleni hapo, ni kukosekana kwa vitendea kazi ikiwemo chaki za kuandikia pale mwalimu anapokuwa darasani akifundisha wanafunzi, hali ambayo ilisababisha watoto hao kukaa katika kipindi cha wiki tatu bila kufundishwa.


Mwanafunzi Desderia Ndunguru wa darasa la saba alisema, mara nyingi kutokana na mazingira ya shule hiyo kuwa magumu, wakati mwingine wanapokuwa darasani wamekuwa wakiingiliwa na wadudu wa aina mbalimbali wakiwemo nyoka, nge na kenge na kuwafanya baadhi ya watoto washindwe kuhudhuria masomo ipasavyo kutokana na kuogopa wadudu hao.

Desderia aliwaomba viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa kutembelea shuleni na kutatua changamoto zilizopo, ili wanafunzi wapate mazingira mazuri ya kusomea ambayo yatapelekea kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Kwa upande wake akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa UVCCM wilayani humo Njowoka alisikitishwa na mazingira mabovu ya shule ya msingi Nangombo jambo ambalo alisema ni udhalilishaji wa watoto ambao ni taifa la kesho na kwamba aliwataka wazazi, viongozi na watendaji wa wilaya hiyo kujenga tabia ya kutembelea shule zote zilizomo wilayani humo, ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu na wanafunzi.

Njowoka aliwaasa wananchi wa Nyasa ambao wanaishi nje ya wilaya, kusaidia jitihada za maendeleo zinazofanywa na wananchi ili kuimarisha ustawi wa maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Aidha kufuatia changamoto zinazoikabili shule hiyo, Kamanda huyo wa umoja wa vijana aliweza kutoa msaada wa chaki, kalamu za wino vifaa vya michezo na kutoa ahadi ya kununua mashine ya kutengeneza chaki, ili kupunguza tatizo la uhaba wa chaki katika shule za wilaya hiyo.


Hata hivyo kutokana na uchakavu wa majengo ya shule hiyo ambayo inatakiwa kujengwa upya, ili kuweza kuwanusuru wanafunzi kukumbwa na maafa ya kuangukiwa na majengo hayo Kamanda huyo wa vijana, ameahidi kushirikiana na wazazi kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa ambapo yeye atagharimia vifaa vyote vya viwandani.

No comments: