Wednesday, April 8, 2015

KUMBURU AZITAKA HALMASHAURI KUTUNGA SHERIA NDOGO ZA UENDESHAJI CPU

 
Adolph Kumburu, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake na Wadau wa zao hilo, hapa nchini.
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKURUGENZI wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Adolph Kumburu, amesema kuwa msimu wa mavuno ya zao hilo hapa nchini umefunguliwa mapema mwezi Aprili mwaka huu, kutokana na baadhi ya maeneo ambayo yanawahi kuiva zao hilo wakulima waweze kuuza kahawa yao mapema bila kuchelewa.

Aidha msimu huu wa mwaka 2015/2016 bodi imefanya makadirio ya kukusanya tani 60,000 tofauti na msimu wa mwaka 2014/2015 ilikadiria kukusanya tani 44,000 lakini haikufikia lengo hilo, badala yake ilikusanya tani 43,000 tu jambo ambalo alifafanua kuwa lilitokana na baadhi ya maeneo hapa nchini zao hilo kushambuliwa na wadudu waharibifu, na kusababisha kushindwa kufikia malengo husika.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi huyo, alipokuwa kwenye mkutano wa Wadau wa zao la kahawa mkoani Ruvuma, uliofanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo wilayani Mbinga mkoani humo.


Kumburu alieleza kuwa umekuwa ni utaratibu wa bodi, kufanya mkutano kama huo na wadau wa zao la kahawa ili kupata fursa ya kutathimini kama kuna tatizo lolote lililojitokeza katika msimu uliopita, na kuweka mikakati madhubuti ili isiweze kujirudia tena katika msimu ujao.

Vilevile katika mkutano huo, Mkurugenzi huyo aliziagiza Halmashauri za wilaya hapa nchini, maeneo ambako kahawa inazalishwa kuhakikisha kwamba inatunga sheria za uendeshaji wa mitambo ya kuchakata kahawa (CPU), ili zao hilo liweze kuzalishwa katika ubora.

Alifafanua kuwa wakulima kwanza, wapate uhalali wa kutumia mitambo hiyo kwa kile alichoeleza kuwa kahawa nyingi huingia katika soko ikiwa na ubora unaokubalika, na kwa msimu uliopita mikoa ya ukanda wa Kusini na Magharibi wakulima ndio walioongoza kuzalisha zao hilo katika viwango vyenye ubora.

“Wakulima jitahidini mchakate kahawa wenyewe, huku mkizingatia kanuni za kilimo bora ikiwemo taratibu za uzalishaji wa zao hili la kahawa, ili tuweze kukuza kipato chetu na Taifa letu kwa ujumla”, alisema Kumburu.

Kadhalika Kumburu aliongeza kuwa takwimu za uzalishaji zao hilo hapa nchini zinaonesha kushuka kila mwaka, kutokana na wakulima wengi wanaozalisha kahawa wamekuwa hawatumii pembeo za kilimo ipasavyo.

Pamoja na mambo mengine, alisisitiza kuwa ushuru unaokatwa na Halmashauri mnadani Moshi kwa kila kilo ya kahawa inayouzwa, asilimia 20 inapaswa kurudi shambani kwa mkulima kwa lengo la kuboresha zao shambani, ili mavuno yaweze kuongezeka mara dufu zaidi.

Alisema hakuna sekta ya kilimo duniani, ambayo inaweza kusonga mbele bila kuingiza mtaji wa kutosha shambani hivyo kuna kila sababu katika eneo hili muhimu, kutazamwa kwa undani na kuweza kuongeza uzalishaji.

Hata hivyo aliwataka wataalamu wa kahawa waache kukaa maofisini, waende kwa wakulima kutoa maelekezo na kusimamia kanuni bora za kilimo cha zao hilo ili kumsaidia mkulima, aweze kusonga mbele na sio kunufaika watu wachache.

No comments: