Monday, April 13, 2015

NYASA KUMUENZI KAPTENI KOMBA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

JUMUIYA ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, umeazimia kumuenzi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, Marehemu Kapteni John Komba kila mwaka ifikiapo Februari 28 wataandaa matamasha mbalimbali ikiwemo kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.

Aidha siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kuwakusanya, wananyasa waishio nje ya Nyasa, kurejea kwao na kusaidia kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo na maendeleo ya wananchi kwa ujumla ili waweze kuondokana na umasikini.

Kwa kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa maendeleo uliofanywa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kamanda wa jumuiya hiyo ya umoja wa vijana wilayani Nyasa, Cassian Njowoka alisema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo wakati alipokuwa akizungumza kwenye baraza la vijana kata ya Kilosa.


Njowoka alisema, marehemu Komba muda wake mwingi enzi ya uhai wake alikuwa akipigania kwa nguvu zake zote maendeleo ya wananchi wake, wakiwemo vijana ambapo muda mwingi alikuwa akiwahamasisha wajiunge pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali.

“Sisi kama vijana lazima tujitoe kwa nguvu zetu zote kumuenzi, ametufanyia  mambo mengi ambayo tukiyazingatia yatatusaidia kuepukana na umasikini, nawaombeni wazo hili liungwe mkono na wananyasa wote”, alisema Njowoka.

Alisema mwaka huu unatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu, hivyo vijana wanapaswa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wale ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, ambapo jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.

Njowoka alisema jumuiya ya vijana ni tegemeo kubwa katika kufanikisha ushindi wa chama, hasa nyakati za chaguzi hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanakuwa na mshikamano wa dhati na kwamba, wasaidie kutangaza kwa wananchi yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo kama ilivyoainishwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema vyama vya upinzani, siku zote vimekuwa na kawaida ya kuwatumia vijana kwa kuwadanganya wakiuke sheria za nchi ikiwemo kuandamana bila kibali halali, huku wao wenyewe wakirudi nyuma, jambo ambalo mwisho wake husababisha vijana hao kukumbana na matatizo makubwa ikiwemo hata kupelekwa mahakamani.


Kamanda huyo wa vijana wa wilaya ya Nyasa, alisema wakati umefika sasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini pia wahamasishe wale ambao sio wanachama wa CCM wajiunge ili kuongeza idadi ya wanachama.

No comments: