Tuesday, April 21, 2015

SERIKALI YATAKIWA KUTOA KIBALI KWA TAASISI BINAFSI KUSAMBAZA RASIMU YA PILI YA KATIBA

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

SERIKALI hapa nchini, imetakiwa kutoa kibali kwa taasisi binafsi ziweze kushiriki kikamilifu kuchapisha nakala za rasimu ya pili ya katiba inayopendekezwa, ili zisambazwe kwa wingi na kumfikia kila mwananchi kwa wakati, hatimaye waweze kuisoma na kuielewa na baadaye waipigie kura ya maoni wakiwa na taarifa sahihi.

Hayo yalisemwa na mtafiti wa maswala ya katiba hapa nchini, Gelin Fuko kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu wakati alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara Mbinga mjini mkoani Ruvuma, uliofanyika kwenye viwanja vya soko kuu mjini humo.

Aidha Fuko aliwataka wananchi wakati utakapofika katika maeneo yao, wajiandikishe kwenye daftari la wapiga kura jambo ambalo litawafanya waweze kuingia kwenye mchakato huo, wa kuipigia kura rasimu hiyo.


“Ndugu zangu msidanganyike kuwa umekumbukwa ilhali hata hujasoma katiba hii inayopendekezwa, nawaombeni kabla ya kuipigia kura hakikisheni umeiosoma na kuielewa ili muweze kutoa maamuzi yaliyo sahihi”, alisema.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi nao kwa nyakati tofauti walitoa maoni yao katika mkutano huo, ambapo walionesha kuiponda rasimu hiyo ya pili ya katiba wakisema kuwa baadhi ya Wabunge wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, wameichakachua katiba hiyo na kuingiza maoni yao na sio yaliyopendekezwa na wananchi.

Walisema hali hiyo imetokana na serikali iliyopo madarakani, kunga’ng’ania mfumo ambao wananchi hawaridhishwi nao hivyo katiba hiyo inanyima haki wananchi kikatiba, na kutaka kupitisha mambo kiujanja ujanja.

Kadhalika walifafanua kuwa wao wanachotambua ni kwamba maoni ya awali yaliyotolewa kupitia timu ya Jaji Warioba, ndiyo wanayoyatambua lakini wanaishangaa serikali kuingiza maoni ya kwake ambayo yanalenga kuwavuruga wananchi.


Hata hivyo kituo cha sheria na haki za binadamu, kinaendelea na ziara yake ya kikazi kutoa elimu kwa wananchi juu ya rasimu hiyo ya katiba hapa mkoani Ruvuma, katika wilaya ya Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru.

No comments: