Sunday, March 29, 2015

MEYA MANISPAA SONGEA ABURUTWA MAHAKAMANI NA TAKUKURU

Charles Mhagama, Meya wa Manispaa ya Songea.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

CHALRES Mhagama, ambaye ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ameburutwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Songea mkoani humo kwa kosa la kutoa rushwa, ikiwa ni lengo la kupora kiwanja cha Ofisa mtendaji wa kata ya Matogoro.

Akisomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu, Elizabeth Missana na Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Greigory Joseph alisema mwaka 2010 katika kata hiyo, Mhagama alitoa shilingi 250,000 na kumpatia Shaibu Ngonyani kama kishawishi cha kumwandikia mkataba feki wa mauziano ya kiwanja hicho.

Mwendesha mshataka huyo aliendelea kudai Mahakamani hapo kuwa, Mhagama alikuwa akitoa fedha hizo akiwa ni Diwani wa kata ya Matogoro ambapo kosa la kutoa rushwa aliloshtakiwa nalo, ni kinyume na kifungu namba 15 kidogo 1B cha sheria ya uzuiaji na upambanaji wa rushwa namba 11 cha mwaka 2007.

Joseph aliieleza Mahakama kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na taasisi ipo tayari kuendelea na shauri hilo, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.


Kesi hiyo ni jinai namba 38 ya mwaka 2015, ambapo mshtakiwa amekana mashtaka yupo nje kwa dhamana ya maneno shilingi 250,000 na kwamba itasikilizwa tena Aprili 16 mwaka huu.

No comments: