Saturday, March 21, 2015

MWAMBUNGU: AMKENI NA KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akisisitiza jambo katika kikao hicho mjini Tunduru mkoani humo.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amewataka Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo, kuamka kutoka usingizini na kuanza kazi ya kukabiliana na changamoto ya utoro na mdondoko mkubwa wa wananfunzi ambao wamekuwa hawaendelei ipasavyo na masomo, katika shule za msingi na sekondari.

Mwambugu alitoa agizo hilo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Wadau wa tathimini ya elimu mkoni Ruvuma, uliofanyika kwenye ukumbi  wa Klasta ya walimu tarafa ya mlingoti mjini Tunduru na kuhakikisha watoto wote wanaoandikishwa, wanamaliza elimu ya msingi na kundelea na masomo ya sekondari.  

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, takwimu zinaonesha kuwa mkoa huo unakabiliwa na mdondoko wa kutisha ambapo mwaka 2008 ulindikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 41,789 lakini takwimu za wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, mwaka 2014 walikuwa 27,771 sawa na asilimia 66. 


Alisema kwa mujibu takwimu hizo watoto 14,018 walipotea mitaani hawakuhudhuria masomo, hali ambayo alisema kwamba haivumiliki na kuendelea kufumbiwa macho na kuacha vijana hao ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa hili,  wakiangamia kwa kukosa maarifa.

“Haiwezekani tuache watoto wakizagaa mitaani, huku viongozi tuliopewa mamlaka tukiendelea kupokea mishahara, huku tukiwa hatutimizi wajibu wetu ipasasvyo”, alisema.
Kufuatia hali hiyo, Mwambungu aliwataka viongozi hkatika mkoa huo kujenga ushirikiano kutoka ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa na kata kwa kuchukua majukumu ya kuhakikisha watoto wote walioandikishwa wanahudhuria masomo darasani kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Alisema endapo kutakuwa na kikwazo cha aina yoyote ile kutoka kwa mzazi husika, ni wakati wa kuwafikisha mahakamani ili hatua stahiki zichukuliwe na kuondokana na tabaka la watoto ambao hawataki kwenda shule.

Katika kuhakikisha kwamba mkoa huo, unasonga mbele kitaaluma maafisa elimu wameagizwa waliopo ndani ya mkoa wanapanga utaratibu kuwa, walimu katika shule zote wanapaswa kufanya kazi katika eneo lolote, yakiwemo maeneo ya shule zilizopo vijijini.

Akitoa taarifa ya hali ya elimu mkoani humo, Afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Mayasa Hashim alisema pamoja na kuwepo kwa upungufu wa miundo mbinu kwa mwaka 2014 mkoa huo, uliweza kufaulisha jumla ya wanafunzi 15,209  na kuongeza idadi ya ufaulu wa asilimia 16 baada ya kufikia asilimia 54 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2013.

Idadi hiyo inatokana na mkoa kusajili watahiniwa 28,418 ambapo kati yao wanafunzi 27,711 walifanya mtihani huo na kwamba mchanganuo unaonesha kuwa kati ya  watoto hao waliofaulu, watoto 116 walichaguliwa kwenda kujiunga katika shule maalumu na wengine waliobakia walipelekwa kwenda kujiunga na masomo ya sekondari, katika shule zilizopo zilizopo hapa mkoani Ruvuma.


Hashimu alifafanua kuwa ingawa ufaulu huo ni mdogo, na ambao umeufanya mkoa huo kutofikia lengo la matokeo makubwa sasa (BRN) la asilimia 66 na kwamba ili kufikia lengo hilo, mkoa wake umejipanga kuhakikisha kwamba wanalifikia katika matokeo ya mwaka huu.

No comments: