Saturday, March 28, 2015

WALIMU MBINGA WALIA WAITAKA SERIKALI IWALIPE MADAI YAO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma, kimesema kwamba walimu wake waliopo wilayani humo, wanaidai serikali shilingi milioni 238,777,267.30 kwa muda mrefu sasa jambo ambalo linawafanya walimu washindwe kuwajibika ipasavyo mashuleni.

Imeelezwa kuwa deni hilo ni la madai mbalimbali ambayo ni malimbikizo, uhamisho, matibabu, likizo, masomo na kujikimu hivyo wameitaka serikali kuhakikisha deni linalipwa mapema ili kuondoa malalamiko miongoni mwao.

Hayo yalisemwa na Katibu mkuu wa CWT wilayani Mbinga, Werner Mhagama alipokuwa akisoma taarifa ya utendaji kazi za chama kwa kipindi cha mwezi Julai 2013 hadi Disemba 2014 kwenye mkutano mkuu wa wilaya, uliofanyika ukumbi wa Uvikambi uliopo mjini hapa.

Mhagama alifafanua kuwa chama pia kimebaini kuwepo kwa tatizo la kutopandishwa vyeo walimu wilayani humo, hasa kwa wale ambao wanasifa ambapo mpaka sasa waliostahili ni 521 lakini waliopandishwa ni 470 tu.


Katibu huyo alieleza kuwa katika kipindi hiki, chama kimekuwa na matatizo ya kutokuwa na maelewano, kati ya uongozi wa CWT na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo hasa pale wanapofanya kazi ya ufuatiliaji wa madai mbalimbali ya walimu.

Alisema ili walimu warudi na kufanya kazi kwa nguvu na ufasaha zaidi, wanaiomba serikali kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri, kuteua wasimamizi makini na kusambaza vifaa vya kutosha shuleni, kuendesha semina kwa walimu ili kuboresha ufundishaji, wanasiasa kutoingilia masuala ya kitaaluma, kuwapandisha vyeo na kuwalipa stahiki zao kwa wakati.

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali ambao watakiongoza chama hicho wilayani Mbinga, katika kipindi cha miaka mitano ambapo nafasi ya Mwenyekiti alichaguliwa Batson Mpogolo aliyepata kura 156 na kuwabwaga wenzake watatu ambao walikuwa wakiwania nafasi hiyo.

Aidha nafasi ya Mweka hazina ilikuwa ikigombewa na watu sita na kwamba Grace Mbelle aliweza kuibuka kuwa mshindi baada ya kupata kura 97, mwakilishi wa walimu wanawake wagombea walikuwa wawili ambapo Akwilina Ndipo aliibuka mshindi kwa kura 197.

Vilevile Hekelius Ndunguru ambaye alikuwa akigombea nafasi ya mwakilishi walimu walemavu aliweza kupata kura 162, ambapo nafasi mbili wagombea walipita bila kupingwa ambazo ni mwakilishi wa uongozi taasisi za elimu ilichukuliwa na Rogatus Mapunda kwa kura 252 na mwakilishi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi, Abraham Chimbuli alipata kura 250.


Mwakilishi kwa shule za msingi walitakiwa wapatikane watu wanne ambapo ilichukuliwa na Marietha Komba aliyepata kura 69, January Kunani kura 48, Philotheus Mapunda kura 47 na Thomas Komba kura 28 na kwamba uwakilishi shule za awali mshindi alikuwa Philotheus Mapunda kwa kura 75, walimu vijana Gaudence Mbunda aliyepata kura 129 na wawakilishi wawili shule za sekondari ilinyakuliwa na Frank Kinunda kwa kura 126 na Januari Turuka aliyeshinda kwa kupata kura 127.

No comments: