Sunday, March 1, 2015

TAARIFA FUPI JUU YA KIFO CHA MBUNGE WA MBINGA MAGHARIBI HII HAPA

Kapteni Komba akiwa Bungeni Dodoma enzi ya uhai wake, akichangia mada mbalimbali.


Kassian Nyandindi na Mashirika mbalimbali ya habari,

MBUNGE wa Mbinga Magharibi, Kapten John Komba ambaye alifariki dunia jana jioni Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye amesikitishwa kutokea kwa kifo hicho.

Mmoja wa watoto wa Komba ambaye aliyejitambulisha kwa jina la Herman alikuwa akizungumza huku analia, kwamba msiba wa baba yake upo nyumbani kwake Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam.

Habari zinasema asubuhi ya Februari 28 mwaka huu, Komba alikwenda kwenye shughuli zake za kikazi kama kawaida lakini baadaye akajisikia vibaya, hivyo akaamua kurudi nyumbani ambako alizidiwa ndipo familia yake ilipoamua kumkimbiza Hospitali ya TMJ, lakini alipopimwa na madaktari ikathibitika kuwa alikuwa tayari ameaga dunia.

Kapteni Komba ambaye pia ni Mkurugugenzi wa kikundi cha maigizo, Tanzania One Theatre (TOT) ambacho kina kikundi cha taarabu na bendi  inayokwenda na mtindo wa Achimenengule, amekuwa akikisaidia sana chama chake, Chama Cha Mapinduzi katika kampeni zake wakati wa uchaguzi kwa kutunga nyimbo za kuhamasisha wapiga kura na kushiriki kupiga live, kwenye majukwaa ya kisiasa.


Alipokuwa Bungeni:

Enzi ya uhai wake alitamani  sana na kufanya juhudi kubwa ili mtindo wa Achimenengule uwe wa kitaifa lakini ikashindikana,  na badala yake Watanzania sasa tuna muziki wa mduara ambao umekuwa kama mtindo wa muziki wetu, kwa sababu zifuatazo.

Kwanza, ni mtindo halisi wa kitanzania uliochipuka kutoka mahadhi ya kimwambao ya Tanzania. 

Pili, ndiyo mtindo pekee uliowahi kutumiwa na bendi nyingi baada ya kuasisiwa na mabingwa wa muziki wetu, wana njenje, the Kilimanjaro band.

Baada ya bendi hiyo kuiasisi kwa mtindo huo, tayari umepigwa na bendi kama TOT Plus, Chuchu Sound, Pamo Sound, Inafrika Band, wana mipasho kadhaa na mwanamuziki mahiri lakini asiyethamini kiwango chake kikubwa cha muziki, Bob Haisa.

Sababu ya tatu ni kwamba mtindo huo umekuwa wa kupigwa na bendi nyingi, vikundi vingi na wanamuziki wengi si kwa kulazimisha, bali kwa mapenzi tu ya mashabiki wa muziki wa Tanzania.

Kapteni Komba awali alikuwa mwalimu wa shule ya msingi kabla ya kuingia Jeshini na kuwa kiongozi wa kikundi cha maonesho cha jeshi na baadaye Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi akamshawishi aachane na jeshi na kujiunga na CCM, wakati wa mfumo wa vyama vingi ulipoanza hapa nchini  mwaka 1992.

“Mzee Mwinyi ndiye aliyenifanya niache jeshi wakati huo nikiwa na cheo cha ukapteni. Aliniomba nikisaidie chama kwa kuanzisha kikundi ambacho lengo lake lilikuwa kukipigia debe CCM,” aliwahi kusema hivyo Kapteni Komba enzi ya uhai wake.

Pia ameshiriki kampeni za marais Ally Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na aliye madarakani hivi sasa, Jakaya Mrisho Kikwete. Alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi hadi kifo kinamchukua.

Licha ya siasa Kapteni Komba alikuwa anamiliki shule na pia alikuwa na biashara kadhaa. Mwaka 2012 Komba aliwahi kupelekwa India kwa matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji wa nyonga, baada ya kupata ugonjwa uliosababisha mifupa kusagana sehemu hiyo ya nyonga.

Baada ya kurejea nchini alisema upasuaji huo ulichukua saa tano na ulifanyika katika Hospitali ya Apollo, India na alikanusha kuwa alikuwa na ugonjwa wa figo na kurejea hapa nchini Julai 27 mwaka 2012. Ugonjwa uliomuua ni shinikizo la damu ambalo lilikuwa likimsumbua kwa muda mrefu.

Marehemu ameacha mjane, Bi Salome, ambaye ni mwalimu kitaaluma na watoto kadhaa.  

No comments: