Tuesday, March 3, 2015

HATIMAYE KAPTENI KOMBA HATUNAYE TENA MAZISHI YAFANYIKA LEO LITUHI WILAYANI NYASA
















Mwili wa Marehemu Kapteni John Komba ukishushwa Kaburini, katika makaburi ya kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Rais Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete, wakiweka shada la maua katika kaburi la Marehemu Kapteni JohnKomba Mbunge wa Mbinga magharibi, wakati wa mazishi leo kijijini Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

WANANCHI wa Jimbo la Mbinga Magharibi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameshindwa kuzuia hisia zao mbele ya Rais Jakaya Kikwete ambaye ameongoza mazishi, pale mwili wa Mbunge wao Kapteni John Komba ulipokuwa ukishushwa kaburini na askari wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wengine wakilia na kusikika wakitamka maneno; tumempoteza mtu muhimu, mpiganaji wa kweli ambaye alikuwa akitusaidia kujenga maendeleo ya jimbo letu, tutampata wapi mtu kama huyu.

Aidha licha ya maneno hayo kutamkwa na wananchi hao, simanzi na majonzi vilianzia katika viwanja vya shule ya msingi Lituhi, eneo ambalo liliandaliwa kwa ajili ya kuuaga mwili wa Mbunge huyo na maombolezo ya sala ambayo yalikuwa yakiongozwa na Askofu wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo ambapo Rais Kikwete hakuweza kuzungumza chochote wakati wa mazishi hayo.

Vilio hivyo viliendelea kutawala ambapo hata Rais Kikwete, vilimfanya aonyeshe huzuni kubwa huku akitumia kitambaa chake kufuta machozi wakati mwili huo unahifadhiwa kwenye makaburi ya kijiji hicho, alichozaliwa Kapteni Komba.

Awali wakati Askofu Ndimbo akiendesha ibada hiyo ya mazishi, aliwataka waumini kuacha matendo ya kumpuuza mwenyezi Mungu, badala yake watende mema katika maisha yao kwani hakuna binadamu aliyefunga mkataba na Mungu, juu ya kuishi hapa duniani.



“Miili yetu ni hekalu la bwana na maskani ya mpito hapa duniani, inatupasa kufanya kila jitihada kwa mambo ambayo yanampendeza Mungu, hakuna binadamu asiyekuwa na utashi juu ya kifo”, alisema Ndimbo.

Kadhalika aliongeza kuwa mwenyezi Mungu, anaouwezo wa kumchukua yule mtu ambaye binadamu walimtegemea kwa namna moja au nyingine hapa duniani, huku akisisitiza waumini kutenda mema kwa yale yote yaliyofanywa na Mbunge huyo.

Akielezea wasifu wa marehemu huyo, alisema kuwa alikuwa ni mtu ambaye tegemeo kubwa kwa wananyasa kupitia huduma zake alizokuwa akizitoa kwa jamii, katika nyanja za kimaendeleo hasa kwa kuijenga wilaya hiyo ambayo ni changa.

Umati mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, wamehudhuria mazishi hayo wakiwemo viongozi wa chama na serikali, ambao walifurika kijijini Lituhi kwa lengo la kumsindikiza aliyekuwa mbunge wao na mwimbaji maarufu, wa bendi ya Tanzania One Theater (TOT).

Viongozi na wananchi walipata fursa ya kuuaga na kutoa heshima zao za mwisho, kwa mpendwa wao Mbunge huyo, marehemu Kapteni Komba.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM) Abdulharman Kinana alisema, tumepoteza kiongozi ambaye anaupendo, mchapa kazi na alikuwa mstari wa mbele kusaidia watu wake.

“Alhamisi iliyopita alikuja ofisini kwangu, tukazungumza akaniambia anataka kupeleka bati jimboni kwake bahati mbaya kafariki, tumepata pigo kubwa, daima tutamkumbuka kwa upendo, uvumilivu na mchango wake mkubwa katika chama”, alisema Kinana.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Ruvuma, Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, alisema walishitushwa na msiba huo mzito kamwe hawatamsahau Kapteni Komba ambaye alikuwa kiongozi jasiri, mkweli na mpenda wapiga kura wake.

Pia salamu kutoka kwa vyama vya upinzania Mbunge wa Lindi (CUF) Salum Buruan, alisema wamepokea kifo hicho kwa masikitiko makubwa kwani alikuwa akimfariji kuwa ipo siku tatizo la mauaji ya Albino litakwisha hapa nchini, wataendelea kuwa salama ambapo hata yeye wakati akiwa Dar es Salaam alikuwa akimhakikishia ulinzi kuwa yupo salama.

“Ndugu zangu wananchi marehemu alikuwa kipenzi cha watu, na hakika ni kiongozi mpenda watu, kambi ya upinzani inasikitika sana kumpoteza kiongozi huyu mahiri na shupavu”, alisema Buruan.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda alisema Taifa limempoteza mpenda wanyonge, huku akiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kujiandaa kwa kusali, pia waache tabia ya kuona mtu aliyekufa kwamba amekosa bali wajenge tabia ya kupendana.

Kapteni Komba alifariki dunia, Februari 28 mwaka huu majira ya jioni katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, wakati akiendelea na matibabu.

No comments: