Tuesday, March 24, 2015

KIGONSERA WAMLALAMIKIA MKURUGENZI WA MBINGA KUTUMIA NGUVU KUCHUKUA MALI ZAO, WASEMA AMEKOSA UTAWALA BORA WATAKA SERIKALI KUINGILIA KATI

Rais Jakaya Kikwete, wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Na Kassian Nyandindi,

HUSSEIN Ngaga, ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, analalamikiwa na Wakazi wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani humo akidaiwa kutumia mabavu kwa cheo alichonacho na kuchukua mali kadhaa za kijiji hicho, kinyume na utaratibu.

Kitendo alichofanya Mkurugenzi huyo kimeelezwa kuwa ni wizi, kutokana na kile walichoeleza kwamba hakuna kikao chochote kilichoketi kijijini hapo na kuridhia achukue mali zao, ambavyo ni vifaa vya thamani walivyokabidhiwa na mkandarasi wa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka pacha ya Peramiho hadi Mbinga mjini, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko miongoni mwa jamii.

Ngaga ananyoshewa kidole na wakazi wa kijiji cha Kigonsera kwamba ametumia nguvu, na kulazimisha kuchukua vifaa hivyo ambavyo walikabidhiwa na mfuko wa barabara wa Millenium Challenge Account (MCA – Tanzania) mara baada ya Mkandarasi, ambaye ni kampuni ya kichina ya Sinohydro Corporation Limited kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mkandarasi huyo ambaye alikuwa ameingia mkataba na kijiji (nakala tunayo) inaonesha na kuthibitisha kuwa alikuwa ametumia sehemu ya ardhi ya kijiji hicho, kwa ajili ya kuweka kambi na kujenga majengo ambayo yalikuwa yakitumika kulala wataalamu wa ujenzi wa barabara hiyo.


Hivyo mara baada ya kukamilisha kazi ya ujenzi, majengo na mali kadhaa zilizomo ndani yake mnamo Januari 15 mwaka 2014 walikabidhiwa kijiji, mbele ya kikao cha baraza la kata (WDC) kwa ajili ya matumizi ya shule ya sekondari Kiamili iliyopo kijijini hapo wilayani humo, ili viweze kuwasaidia walimu wanaofundisha shuleni hapo.

Katika hali ya kushangaza mara baada ya taratibu za makabidhiano hayo kufanyika Mkurugenzi Ngaga kwa siku zilizofuata, alimtuma Ofisa utumishi wake wa wilaya ya Mbinga, Emmanuel Kapinga kwenda kuchukua vitu vya thamani vilivyomo ndani ya majengo hayo, kwa kutumia nguvu bila wananchi wa eneo hilo kujulishwa kupitia vikao halali kitendo ambacho wanasema ni wizi, huku akijua fika mali alizochukua ni za wananchi wa kijiji cha Kigonsera.

Ofisa utumishi huyo baada ya kuwasili katika eneo hilo, anadaiwa kulazimisha kupewa funguo za majengo hayo ambazo zilikuwa zikitunzwa na uongozi husika uliokabidhiwa mali hizo, na alipopewa aliingia ndani ya majengo na kuchukua vitu kadhaa vilivyomo ndani yake na kuondoka navyo.

Pia uchunguzi umebaini kuwa ofisa utumishi Kapinga, alipoingia ndani ya majengo hayo alichukua vifaa vya thamani vifuatavyo; majiko ya umeme 12 na control zake 12 aina ya west point, makabati ya nguo na jikoni jumla yake 34, mitungi ya gesi 10, water friji 2, masinki mapya ya choo 7 pamoja na meza ndogo za kisasa 4.

Mwandishi wetu baada ya kufanya ufuatiliaji wa kina juu ya vitu hivyo vimepelekwa wapi, imebainika kuwa wamegawana vigogo kadhaa wa wilaya ya Mbinga (majina tunayo) na kwenda kuvitumia majumbani kwao, ndio maana leo kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale.

Hata baadhi ya madereva wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambao walishiriki katika mchakato wa kwenda kubeba vitu hivyo, nao walipewa chapuo la kugawiwa baadhi ya vitu kama vile mitungi ya gesi.

Wananchi wa kijiji cha Kigonsera kwa nyakati tofauti wamesikitishwa na kitendo hicho, huku wengine wakieleza kuwa vitu vyote vilivyomo ndani ya majengo hayo wakati kijiji kinakabidhiwa vilikuwa vinalenga juu ya matumizi ya shule.

“Ndugu mwandishi, wakati vifaa hivi vinachukuliwa sisi wenyewe tulikuwa tunashuhudia hapa magari ya halmashauri yakibeba, akiwa na huyu afisa utumishi wamekuja zaidi ya mara tatu kupakia na kuondoka navyo, kwa kweli tunasikitika sana”, walisema.

Waliongeza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mkurugenzi huyo ni kukosa utawala bora, hivyo wamemtaka ahakikishe anavirejesha mara moja ili kuondoa malalamiko haya yaliyopo sasa, na kwamba wameiomba serikali kuingilia kati juu ya suala hili ili mali zao ziweze kupatikana.


Pamoja na mambo mengine, mkurugenzi Ngaga hakuweza kupatikana ofisini kwake baada ya mwandishi wetu kuwasili ofisini kwake, na kuelezwa kwamba yupo safarini Jijini Dar es Salaam  ambapo hata alipopigiwa simu ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizi, ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: