Tuesday, March 17, 2015

HALMASHAURI MANISPAA YA SONGEA KUBURUTWA MAHAKAMANI


Na Julius Konala,
Songea.

KAMPUNI ya Majembe Auction Mart Limited, inakusudia kuifikisha Mahakamani Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa kile kilichoelezwa kuwa imevunja mkataba wa ukusanyaji ushuru (Service Levy) kinyume na utaratibu, jambo ambalo limeisababishia kampuni hiyo, hasara zaidi ya shilingi milioni 70.

Mkurugenzi wa kanda katika kampuni hiyo, Nelson Mwasomola alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juu ya kitendo cha uvunjwaji wa mkataba huo ambao umefanywa na Halmashauri hiyo.

Mwasomola alisema kusimamishwa kwa kampuni yake, kutoendelea na kazi ya ukusanyaji wa ushuru huo kumesababisha kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa fedha kwa kiwango husika kilichowekwa kwa kila mwezi, na kusababisha kuwepo kwa hasasra kubwa. 


Aidha Majembe Auction Mart, ni kampuni ambayo iliomba kazi ya ukusanyaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) na kwa bahati nzuri ilishinda tenda lakini cha kushangaza wamesimamishwa kuendelea na shughuli hiyo, bila sababu za msingi na kuisababishia hasara kubwa, kutokana na gharama ya kuwekeza jambo ambalo limeifanya kushindwa kumudu  kuwalipa mishahara wafanyakazi wake, pamoja na kodi ya nyumba.

Kadhalika alieleza kuwa pamoja na kampuni hiyo kusimamishwa kuendelea na kazi hiyo, cha kushangaza halmashauri ya Manispaa ya Songea imekuwa ikiendelea kukusanya fedha kwa kutumia kibali cha kampuni ya Majembe Auction Mart kinyume na utaratibu, ambapo mpaka sasa halmashauri imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 25 kupitia vielelezo mbalimbali walivyokuwa wakivitumia kukusanyia ushuru kampuni hiyo.

Alieleza kwamba, imekuwa ni mazoea kila kampuni inapoomba kazi na kushinda zabuni hunyang’anywa tenda bila ya kujali gharama za uwekezaji na uendesdhaji jambo ambalo limekuwa likisababisha hasara, na kwamba mbali ya kuandika barua mbalimbali za kutaka ufafanuzi juu ya jambo hilo, mpaka sasa hawajajibiwa chochote.

Kampuni imekusudia kwenda Mahakamani, huku halmashauri hiyo ikiwa imepewa hati ya mashtaka (notisi) ya siku 30 ya kusudio la kufikishwa kwenye chombo hicho cha sheria, na kutolea maelezo kwa maandishi  sababu zilizopelekea kuvunjwa kwa mkataba huo.

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Nachoa Zakaria alipohojiwa na gazeti hili kuhusiana na tuhuma hizo alidai kwamba hazina ukweli wowote ndani yake, na ofisi yake haijatoa barua yoyote kwa kampuni hiyo juu ya kuvunjwa kwa mkataba wa kukusanya ushuru huo.

No comments: