Friday, March 13, 2015

ZAHANATI ILIYOWEKWA JIWE LA MSINGI NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA TUNDURU YATELEKEZWA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI wa kijiji cha Mtengashari, wilayani Tunduru Ruvuma, wamewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kutimiza ahadi yao ya kuwajengea zahanati ya kijiji hicho.

Kilio cha wananchi hao, kilitolewa kwa njia tofauti ikiwemo kupitia nyimbo zao walizoimba kwa mtindo wa kwaya, pamoja na maoni ya mtu mmoja mmoja wakati walipokuwa kwenye sherehe za kukipongeza chama hicho, kupata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umefanyika hivi karibuni.

Wakifafanua taarifa hiyo, walisema wamechukua uamuzi huo wa kufikisha kilio chao katika sherehe hizo kutokana na CCM kuwa na furaha kubwa kupata ushindi huo wa asilimia 75, huku kijiji chao kikipata ushindi wa asilimia 100 kwa wagombea wa nafasi zote, ikiwa ni tofauti na chaguzi zilizopita ambapo walikuwa wakiongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF).

“Tunajua kuwa ahadi ya kujengewa zahanati hiyo imekuwa ikififia kwa muda mrefu sasa, hivyo tunahitaji kujengewa zahanati hii, ili tuondokane na adha tunayoendelea kuipata sasa juu ya matibabu pale tunapougua”, walisema.


Walisema zahanati hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2014, mbali na wananchi kujitolea kufyatua tofari na kutoa michango mbalimbali ya vifaa na fedha taslimu, lakini juhudi hizo zimekuwa zikionesha kutozaa matunda na kusababisha kuta za jengo hilo ambalo limejengwa kwa muda mrefu, kuanza kubomoka katika baadhi ya maeneo.


Mwandishi wa habari hizi, ambaye alikuwa ni miongoni mwa mashuhuda wa uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa zahanati hiyo, ambao ulifanywa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Juma Mswaduku Abubakar, mnamo Oktober 9 mwaka 2006 lakini cha kusikitisha  jengo hilo hivi sasa limekuwa gofu ambalo ni maficho ya wahalifu, wadudu na wanyama.  

No comments: