Sunday, March 29, 2015

MKURUGENZI MBINGA APUUZA AGIZO LA RAIS KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,

AGIZO lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete juu ya kutoondolewa kwa vifaa vya thamani katika shule ya sekondari ya wasichana Mbinga mkoani Ruvuma, limepuuzwa na vifaa husika vimeendolewa katika majengo ya shule hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga ndiye anayenyoshewa kidole kutumia nguvu kwa cheo alichonacho na kuchukua vifaa hivyo huku akijua fika, Rais Kikwete alikwisha toa agizo vitu vilivyomo ndani ya majengo ya shule hiyo visiondolewe.

Hivi karibuni, Rais Kikwete mnamo Julai 19 mwaka 2014 alikuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga, ambapo alitoa agizo hilo akilenga vifaa hivyo viweze kuwasaidia walimu na wanafunzi ambao wanasoma katika shule hiyo.


Kitendo hicho kilichofanywa na Mkurugenzi wa wilaya hiyo, kimeelezwa kuwa ni wizi na kudharau agizo la mkuu wake wa nchi, hivyo anapaswa kuchukuliwa hatua ikiwemo kurudisha mali alizochukua, ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia ya kupora mali za umma kwa kutumia nguvu.

Aidha imeelezwa kuwa hakuna kikao chochote kilichoketi na kuridhia achukue mali za shule hiyo, ambavyo ni vifaa vya thamani walivyokabidhiwa na mkandarasi wa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka pacha ya Peramiho hadi Mbinga mjini, jambo ambalo limekuwa likizua malalamiko miongoni mwa jamii.

Ngaga ananyoshewa kidole kwamba ametumia nguvu, na kulazimisha kuchukua vifaa hivyo ambavyo wananchi wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera wilayani humo, walikabidhiwa na mfuko wa barabara wa Millenium Challenge Account (MCA – Tanzania) mara baada ya Mkandarasi, ambaye ni kampuni ya kichina ya Sinohydro Corporation Limited kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mkandarasi huyo ambaye alikuwa ameingia mkataba na kijiji hicho (nakala tunayo) inaonesha na kuthibitisha kuwa alikuwa ametumia sehemu ya ardhi ya kijiji, kwa ajili ya kuweka kambi na kujenga majengo ambayo yalikuwa yakitumika kulala wataalamu wa ujenzi wa barabara hiyo.

Hivyo mara baada ya kukamilisha kazi ya ujenzi, majengo na mali kadhaa zilizomo ndani yake mnamo Januari 15 mwaka 2014 walikabidhiwa kijiji, mbele ya kikao cha baraza la kata (WDC) kwa ajili ya matumizi ya shule ya sekondari Kiamili iliyopo kijijini hapo wilayani humo, ili viweze kuwasaidia walimu wanaofundisha shuleni hapo.

Mkurugenzi Ngaga kwa siku zilizofuata, alimtuma Ofisa utumishi wake wa wilaya ya Mbinga, Emmanuel Kapinga kwenda kuchukua vitu vya thamani vilivyomo ndani ya majengo hayo, kwa kutumia nguvu bila wananchi wa eneo hilo kujulishwa kupitia vikao halali kitendo ambacho wanasema ni wizi, huku akijua fika mali alizochukua ni za wananchi wa kijiji cha Kigonsera.

Ofisa utumishi huyo baada ya kuwasili katika eneo hilo, anadaiwa kulazimisha kupewa funguo za majengo hayo ambazo zilikuwa zikitunzwa na uongozi husika uliokabidhiwa mali hizo, na alipopewa aliingia ndani ya majengo na kuchukua vitu kadhaa vilivyomo ndani yake na kuondoka navyo. 

Pia uchunguzi umebaini kuwa ofisa utumishi Kapinga, alipoingia ndani ya majengo hayo alichukua vifaa vya thamani vifuatavyo; majiko ya umeme 12 na control zake 12 aina ya west point, makabati ya nguo na jikoni jumla yake 34, mitungi ya gesi 10, water friji 2, masinki mapya ya choo 7 pamoja na meza ndogo za kisasa 4.

Mwandishi wetu baada ya kufanya ufuatiliaji wa kina juu ya vitu hivyo vimepelekwa wapi, imebainika kuwa wamegawana vigogo kadhaa wa wilaya ya Mbinga (majina tunayo) na kwenda kuvitumia majumbani kwao, ndio maana leo kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale.


Hata baadhi ya madereva wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambao walishiriki katika mchakato wa kwenda kubeba vitu hivyo, nao walipewa chapuo la kugawiwa baadhi ya vitu kama vile mitungi ya gesi. 

No comments: