Tuesday, March 17, 2015

WAUMINI NAMTUMBO WAMPONGEZA MWEKEZAJI KWA KUWAJENGEA MSIKITI




Na Julius Konala,
Namtumbo.

WAUMINI wa dini ya Kiislam, katika kijiji cha Likuyu Sekamaganga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamempongeza na kumshukuru mwekezaji wa kampuni ya Game Frontiers Tanzania (GFT) inayojihusisha na uwindaji wilayani humo, Sheni Abdalah kwa jitihada zake za kujitolea kusaidia ujenzi wa msikiti wa kisasa kijijini hapo, kwa gharama ya shilingi milioni 40.

Pongezi hizo zilitolewa juzi na baadhi ya waumini wa dini hiyo, walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wakidai kwamba kufanikiwa kwa ujenzi huo, kumewaondolea adha pale wanapohitaji eneo la kufanyia ibada.

Immam wa msikiti huo, Omary Kudelega alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kumetokana na maombi ya kujengewa msikiti , yaliyotolewa na waumini wa dini ya kiislam wa kijiji cha Likuyu Sekamaganga kwa mwekezaji huyo.


Kudelega alisema Sheni baada ya kukubali ombi la waumini hao, ndipo alianza kusaidia vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo bati, sementi, boriti, mawe, mchanga na kuwafungia nishati ya umeme msikitini hapo, inayotokana na nguvu ya jua (Sola). 

Alieleza kuwa kukamilika kwa msikiti huo, kumekuwa ni mkombozi mkubwa kwao kutokana na awali waumini wa eneo hilo walikuwa wakifanya ibada kwenye jengo bovu, hali ambayo ilikuwa ikiwasababishia baadhi yao kuswalia nje, huku wakati mwingine wakinyeshewa na mvua kipindi cha masika.

Msikiti huo wenye uwezo wa kuchukua waumini kuanzia 300 hadi 400 umekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa kijiji hicho, wageni, wasafiri pamoja na baadhi ya watumishi wanaofanya utafiti wa madini aina ya uranium, katika mradi wa mto Mkuju.

Hata hivyo waumini hao wamemwomba Mwekezaji huyo, kuendelea kuwasaidia ujenzi wa nyumba ya kuishi Immam wa msikiti huo, ofisi ya Bakwata, pamoja na darasa kwa ajili ya kuwafundishia waumini wa dini hiyo. (Madrasa)

No comments: