Monday, March 9, 2015

SIASA BILA DINI NI UWENDAWAZIMU

Padre Baptiste Mapunda.
Na Padre Baptiste Mapunda,

HISTORIA ya siasa duniani, haitengani sana  na  historia ya dini. Vitu hivi  viwili kwa maisha ya mwanadamu, vimekuwa sambamba na vyenye mafao kwa jamii yoyote ile duniani ambapo kwa upande mwingine dini na siasa vimeleta matatizo makubwa hapa duniani.

Uhusiano mzuri usipojengwa kati ya siasa na dini, hakika katika dunia hii na nchi yetu kwa ujumla tutaendelea kushuhudia machafuko na uharibifu mkubwa wa  mali, pamoja na mauti dhidi ya binadamu kama yalivyowahi kutokea hapa nchini hasa katika kampeni za kisiasa. Mara nyingi maovu hayo, yanasababishwa na uelewa mdogo juu ya mahusiano ya siasa na dini.

Na hivi sasa Tanzania imezalisha ugonjwa mpya unaojulikana kwa jina la “udini.” Unapoanza kuingiza udini katika ajira, elimu, afya  na siasa ujue kwamba  usalama wa nchi huenda ukawa hatarini.

Kutenganisha kabisa siasa na dini ni kitu ambacho hakiwezekani katika dunia ya leo, bali kinachotafutwa ni kila taasisi kuielewa vyema inahusiana vipi na nyingine, na kutengeneza mipaka yake na leo hii ndiyo ninaandika kwamba; “siasa bila dini ni uwenda wazimu.”


Huwezi kusema wewe unashughulika na siasa, halafu ukajidanganya  kwamba hauhusiki na masuala ya dini, wananchi  wengi ni waumini wa madhehebu mbalimbali mathalani kwa nchi ya Tanzania kuna waislamu, wakristo, wabudha, wahindu, na hata wapagani.

Siasa ambayo haigusi maisha ya waumini, inakuwa imejitenga na jamii husika na kitu muhimu na kinachotakiwa hapa, ni busara kujenga mahusiano mazuri kati ya nyanja hizi mbili bila kuwepo njia potofu.

Katika siasa za Tanzania, nimegundua kuanzia kelele za muda mrefu zinazotolewa na serikali, pamoja na wanasiasa kuwataka viongozi wa kiroho au dini wasichanganye dini na siasa, hapa nasema hakuna msingi wowote ule kutokana na mambo hayo mawili, hayawezi kutenganishwa kabisa.

Wanaoshikilia msimamo huo, wanaonyesha woga wa juu na uelewa finyu katika masuala ya dini na siasa, hii ni bahati mbaya.

Kwa sisi wakristo tunasema, Yesu Kristo hakuhubiri habari za ufalme wa Mungu tu na kuacha dhambi, bali aligusa maswala ya jamii kama amani, umaskini, kutenda haki, mahusiano mazuri, madhara ya rushwa na ufisadi, wizi wa mali ya umma, utunzaji wa rasilimali  na hata kuponya magonjwa na hii ndiyo injili sahihi yaani injili ya jamii.

Yesu alikuwa akihubiri  injili ya jamii na sisi je haitupasi kuhubiri injili hiyo hiyo ya jamii? Je, viongozi wa serikali  na wanasiasa msingi wa hofu yao juu ya viongozi wa kiroho, kuongelea masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada ni  nini?

Wiki jana kanisa katoliki, lilitoa msimamo wake kuhusiana na kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania, kupitia tume ya haki na amani kwa ushirikiano na CPT  wametoa waraka au tamko ikipendekeza kusitishwa kwa mchkakato wa kura ya maoni, ili kupisha maandalizi mazuri ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, je hapo kanisa limefanya siasa?

Ni wajibu wa kanisa kama chombo cha wokovu kwa wanadamu wote, na kiongozi wa imani na jamii kufanya kazi yake hii ya kinabii, sura ya nne ya ujumbe wa Maaskofu katoliki wa kwaresma mwaka huu, ambapo nakala yake ninayo hapa mezani unaongelea “wajibu wa kijamii wa kanisa”. Sehemu hii inasema kwamba; kila mara kanisa linapotimiza wajibu huu linashutumiwa kuingilia siasa ambapo tafsiri hiyo nasema ni potofu.

Kamwe kanisa katoliki haliwezi kukaa pembeni, kwani litakuwa linafanya dhambi ya kutotimiza wajibu wake kwa jamii. Injili ya Yesu ambayo ni ya upendo, amani na umoja lazima ihubiriwe kwa kila mtu  katika jamii husika, kwa mfano Yesu anafundisha tuache siasa za jino kwa jino.

Katika ujumbe huu wa kwaresima Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere amenukuliwa kwamba aliwahi kuliasa kanisa akisema, “iwapo kanisa  halitashiriki kwa vitendo katika maasi dhidi ya mifumo dhalimu ya kiuchumi inayosababisha watu, kutoswa katika fedheha ya  umaskini na kudhalilishwa, kanisa halitakuwa na maana yeyote kwa watu na dini ya kikristo itapoteza mvuto na kuwa kama ushirikina, jambo hili likitokea, kanisa litakufa.”

Katika jamii ya Kiyahudi enzi za kale, manabii walikuwa wanaishi ikulu pamoja na mflame  wao, kwa lengo la kumsaidia  mfalme katika kazi yake  ya kuongoza jamii. Ni nabii aliyekuwa anampaka mafuta mfalme ili mkono wa Mungu, nguvu, na hekima iwe naye katika kazi yake ya kuhudumia jamii nzima bila ubaguzi.

Tanzania ya leo inahitaji manabii, kama alivyojitokeaza Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Lakini pia ni wajibu mkuu wa viongozi wa dini kuwasaidia viongozi wa serikali na wanasiasa ili waweze kuwa na roho ya Mungu katika uongozi wao na ndiyo maana nasema, siasa bila dini ni uwenda wazimu.”

Ikumbukwe kuwa enzi za kale wakati wa uteuzi wa kiongozi wa jamii, mtu aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo mara nyingi, alikuwa ni yule aliyeonekana ni mcha-Mungu na watu walimuamini ataweza kuongoza vyema kwa sababu, sauti ya Mungu ilikuwa ndani yake. Mimi naamini Nyerere alikuwa kiongozi bora kwa sababu alikuwa pia na uchaji wa Mungu.

Kuipotosha jamii kwamba, viongozi wa dini hawana uhusiano na mambo ya kisiasa ni kutowatendea haki ni lazima tutambue kwamba viongozi wa dini ni viongozi wa jamii pia. Mimi ningependa kujua je, mpaka wa dini na siasa upo wapi, ndiyo maana mimi naamini kwamba siasa bila dini ni uwenda wazimu hivyo wananchi wanaohutubiwa katika mikutano ya kisiasa majukwaani siku ya ibada wanakuwa waumini wetu.

Kutaka kuwatenganisha viongozi wa dini na siasa, ni kutaka kujenga chuki kati ya waumini na viongozi wao, mwisho napendekeza kwamba viongozi wa serikali na wanasiasa wa vyama vyote lazima waepuke kuwapotosha waumini wetu, na kuwajenga chuki na viongozi wa madhehebu yao.

Mungu ibariki Afrika, Tanzania  na watu wake.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com

No comments: