Wednesday, March 18, 2015

PROFESA SIGALLA ALIA NA WATUMISHI MANISPAA YA SONGEA

Na Julius Konala,
Songea.

MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Profesa Norman Sigalla amewataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha, ikiwa ni lengo la kuimarisha utendaji kazi kwa manufaa ya jamii, na upambanaji wa vita dhidi ya watu wenye tabia chafu ya kukatisha maendeleo ya wanafunzi masomo darasani hususani kwa watoto wa kike, kuwapa ujauzito.

Sigalla alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na watumishi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia na wakuu wa idara  wa halmashauri hiyo kwenye ukumbi wa mikutano uliopo, ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kwa lengo la kufamihana.

Alisema hatakuwa na huruma wala kumfumbia macho, mtumishi yeyote atakayebainika anaendesha vitendo viovu, huku akiapa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, sambamba na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

“Natoa onyo hata kwa wazazi na walezi, ambao watakabainika kushindwa kutoa ushirikiano kwa serikali yetu katika kuwafichua watu ambao wamewapa ujauzito watoto waliokatika wakati wa kwenda shule, kwa sababu ya kurubuniwa na fedha au kitu fulani kwa lengo la kupoteza ushahidi, hatua kali za kisheria  zitachukuliwa dhidi yao”, alisema Sigalla.


Aidha amewataka watumishi hao wa halmashauri ya Songea, kutumia muda mwingi kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo na kuwatumikia wananchi badala ya muda mwingi kukaa na kupigana majungu, jambo ambalo amedai kuwa ni adui mkubwa wa maendeleo katika halmashauri yoyote ile.

Vilevile kwa upande wa watumishi waliobahatika kuwa na elimu na nyadhifa za juu, katika halmashauri hiyo waache tabia ya kujifanya miungu watu kwa kunyanyasa na kudharau wenzao ambao wana elimu  ndogo, kwa madai kwamba wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja anamchango na thamani yake katika jamii.


Hata hivyo, Profesa Sigalla amehamishiwa katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kuendelea na wadhifa wake wa kuwa mkuu wa wilaya hiyo akitokea wilaya ya Mbeya baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko na uteuzi wa wakuu hao miezi michache iliyopita.

No comments: